NA BASHIR YAKUB-WAKILI
KIPINDI cha nyuma wakati nikieleza masuala ya sheria za ndoa niliwahi kueleza utaratibu wa mgawanyo wa mali iwapo ndoa inavunjika. Kimsingi nilieleza mgawanyo wa mali katika msingi wa uwepo wa ndoa ya mke mmoja. Sikuwahi kueleza mgawanyo wa mali iwapo ndoa ni ya mke zaidi ya mmoja. Wengi waliuliza swali hili ambapo baadhi niliwajibu na baadhi sikuwajibu. Leo sasa nitaeleza mgawanyo wa mali katika ndoa ya mke zaidi ya mmoja pale ambapo mmoja wa wake inatalakiwa .
1.NDOA YA MKE ZAIDI YA MMOJA.
Kwa jina la kitaalam ndoa za namna hii huitwa ndoa za mitala. Waolewaji waweza kuwa wawili, watatu , wanne, watano au zaidi neno mitala hubaki kuwa mitala. Sheria yetu ya ndoa inatambua ndoa ya mke zaidi ya mmoja na hivyo kwa waliofanya hivyo hawajatenda dhambi yoyote kisheria. Ndoa za namna hii mara nyingi zimekuwa zikifungwa na waislamu au watu ambao huishi maisha ya kufuata mila ambao wengi wao wako vijijini. Hata hivyo tumeshuhudia mazingira ya ndoa za namna hii kwa watu ambao ni wa makundi tofauti na niliyotaja kwa siku za hivi karibuni. Yote kwa yote hizo ndio ndoa za mitala.
2.ISEMAVYO SHERIA YA NDOA KUHUSU MKE ZAIDI YA MMOJA.
Kifungu cha 57 cha sheria ya ndoa kinaweka wazi kwa kusema kuwa, katika sheria yoyote ile mwanaume anapokuwa na wanawake wawili au zaidi wanawake hao wanatakiwa kuwa na haki sawa mbele ya macho ya sheria na si vinginevyo. Kawaida tumezoea kuna u bi mkubwa na u bi mdogo. Basi ieleweke kuwa hayo ni mambo ya kwetu lakini sheria haina u bi mkubwa wala u bi mdogo. Sheria inajua mke ni mke awe alianza kuolewa au ameolewa mwishoni. Wake wote wana haki sawa mbele ya mme wao na mbele ya sheria na huo ndio msimamo wa sheria.
3.MGAWANYO WA MALI UKOJE IWAPO MKE MMOJA AMETALAKIWA.
Katika hili msimamo wa sheria ni kuwa japo wanawake ni wengi na mtu aliyewaoa ni mmoja bado kila mwanamke ana mgao wake ambao uko tofauti na mwingine iwapo ndoa ikivunjika. Hapo juu tumeona sheria ikisema wanawake walioolewa na mme mmoja wana haki sawa. Ni kweli wana haki sawa lakini ili haki sawa ipatikane ni lazima baadhi ya mambo ya msingi yazingatiwe. Ili mke fulani amzidi mwingine katika mgao wa mali ndoa inapovunjika kitu kikubwa kinachozingatiwa ni mchango wake katika upatikanaji wa mali zilizopo.
Ikiwa mchango wa mwanamke fulani ni mkubwa basi atachukua kikubwa na ikiwa mchango wake ni mdogo basi atachukua kidogo. Kubwa zaidi ni kuwa kila mwanamke atachukua kile kinacholingana na mchango wake katika upatikanaji wa mali husika. Katika mgawanyo wa mali za ndoa sheria haikuweka msimamo wa kiasilimia kama ilivyo katika mambo mengine ya mirathi n.k. Katika hili sheria humtaka kila mhusika kuthibitisha amechangia nini ili apate haki yake kutokana na mchango huo.
4. BI MDOGO ANAWEZA KUPATA MALI NYINGI KULIKO BI MKUBWA.
Kwa msimamo wa nilichoeleza hapo juu basi yawezekana bi mdogo akapata mali nyingi kuliko bi mkubwa iwapo ndoa yake itavunjika.
Yawezekana bi mdogo ameolewa miaka kiwili tu lakini lakini fedha yote ya kujengea nyumba za familia imetoka kwake au nusu yote imetoka kwake au kiasi cha pesa kilicholeteleza upatikanaji wa viwanja na magari n.k. kilitoka kwake. Na ikawa bi mkubwa pamoja na kukaa kwenye ndoa zaidi ya miaka thelathini lakini mchango wake ni mdogo au ni wa kawaida ambapo hakuwahi kuchangia chochote zaidi ya mchango wake wa kazi za nyumbani. Kimsingi mchango wa kazi za nyumbani ni mchango na unatambulika isipokuwa kwa mazingira niliyoeleza hapa mchango huo hauwezi kustahili mgao sawa na wa bi mdogo aliyetoa pesa yote au nusu mpaka mali hizo zikapatikana.
Nimalizie kwa kukumbusha kuwa kitu kikubwa kinachozingatiwa katika kugawana mali iwapo ndoa ya mke zaidi ya mmoja imevunjika ni kuangalia mchango wa kila mmoja au mchango wa anayeondoka katika juhudi za upatikanaji wa zile mali. Kila mtu atachukua kulingana na mchango wake baada ya kuudhibitisha.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI NA SERIKALI LA HABARI0784482959,0714047241 bashiryakub@ymail.com
0 Comments