UNAZIKUMBUKA SAFARI ZA TRENI ENZI ZILE?
Kwa kweli inatubidi tu kwenda na usasa na kusahau yale ya zamani. Ndio, treni ya SGR ina usasa mwingi kuliko ile yetu ya zamani.
Ina kasi sana na mtu unawahi kufika unakokwenda na ndani yake kuna usasa mwingi. Mbali na zamani kuchelewa kufika lakini pia tulikuwa hatutangaziwi vituo. Ilikuwa ukitaka kujua ulipo unatoa kichwa nje na kuangalia mazingira, au unasubiri ukifika kwenye kituo kinachofuata ndio unajua kama ni Godegode au Kazuramimba. Wengine tulikuwa tunatumia saa, tumetoka Mwanza saa kumi na mbili, muda huu tutakuwa tunakaribia Shinyanga. Madereva wa treni yetu tuliwajua kutokana na mwendo wao, yaani jinsi walivyokuwa wakiendesha!
Lakini acha niseme ukweli, pamoja na maboresho ya hali ya juu, kuna vitu sisi tuliopanda treni yetu ya zamani tunavimisi sana.
Zamani tulikùwa tunapanda na chakula chetu kwenye treni, siku hizi marufuku, umekaangiwa nyama, chapati na mchuzi unapewa na chupa ya chai. Chai yako ikiisha njiani kuna watu wanauza chai.
Binafsi nimemisi zile kelele za "Chai....Chai....Chai..."
Unakumbuka treni ilipokuwa ikifika Salanda? Nanì ameyasahau yale mapaja ya kuku manene na marefuuu... Hebu tuulizane vizuri, "Hivi walikuwa kuku kweli wale?"
Siku hizi huapandi hata na maji ya kunywa, kwasababu yapo ndani, robo lita yanauzwa buku. Hata crips na korosho zinauzwa ndani, bei yake unajiuliza mara mbilimbili, ninunue au nisinunue...?
Chai iko kwenye kile kikombe cha take away, haitoshi hata kumalizia chapati moja.
Treni yetu ilikuwa na mabehewa ya kitajiri na kimasikini, yaani first class, second class na third class. Pia, kulikuwa na second sitting lakini hakukuwa na mtu wa kukuzuia kupanda na dumu la lita tano za maji.
Lakini hii treni ya sasa ni ya kitajiri zaidi pamoja na kutenganishwa kwa Business class na Economy, unaweza kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na kachupa kako ka maji, labda kwasababu tunachukua muda mchache kufika. Utakula ukifika...
Lakini safari ni bonge la mtoko, unapaswa kula, kunywa na kuifurahisha nafsi, lakini je, utamudu gharama?
Nimeikumbuka ile treni yetu ya kijamaa, treni ya uhuru mnakaa chumba kimoja watu sita, mnalala na kuamka wala hakuna shida. Mtu unakuwa na uhuru mkubwa wa kuinjoi na kuifurahia safari .
Hivi hii treni yenu mtakuwa na mabehewa ya kulala ikifika Mwanza? Nimeuliza tu wadau maana nimemisi makelele na sauti za kutangaza bidhaa pindi treni ilipokuwa ikifika kituoni. Najua wachache ndio watakaonielewa.
Iko wapi ile treni yetu?
-MO Kuyunga

0 Comments