HALE FESTIVAL IMEITIKA, IMEBAKI 'KUMFUFUA' TX MOSHI



BABU yenu Kionambali M.Kionambali(87) tayari nipo Hale, Korogwe Mkoani Tanga.Kilichonileta hapa ni tukio kubwa kabisa la burudani lililopewa jina la Hale Festival ambalo ndani yake kuna kumbukizi ya aliyekua gwiji wa muziki wa dansi  marehemu Ally Muhoja Kishiwa TX Moshi William.

Uhondo  huo utafanyika Desemba 26, 2025  'Boxing Day' ndani ya Hale Lounge ambapo tukio limeandaliwa na mjukuu na rafiki yangu Dk.Hassan Abassy mmoja ya wadau wakubwa wa muziki wa dansi nchini na masuala ya sanaa.

Tangu nimeingia Hale nimepata nafasi ya kutembea kidogo mtaani kama njia ya kunyoosha miguu na kujionea mandhari nzuri ya mji huu ambapo nimekutana na kundi kubwa la wageni kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu.Kilichowaleta hapa ni Hale Festival ambapo bendi kubwa mbili za dansi nchini Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' na Mlimani Park Orchestra 'Sikinde Ngoma ya Ukae' zitaoneshana kazi  jukwaani.

Vijiwe mbalimbali vya kahawa nimekuta mjadala ni tukio hilo kubwa la burudani kuandaliwa kwa mara ya kwanza ndani ya mji wa Hale.Hakika mambo ni moto kuelekea Hale Festival ambapo utakua usiku wa kumfufua' TX Moshi William kama njia ya kuonesha kutambua/kuthamini mchango wake alioutoa kupitia tungo zake akiwa na Polisi Jazz Band na Msondo Ngoma.

Nimepita nyumba kadhaa za wageni 'Guest House' na kukutana na vibao vimeandikwa VYUMBA VIMEJAHii ni ishara  Hale imevamiwa na Hale Lounge kesho lazima itatapika mamia ya watu waliokuja kwa ajili ya tamasha hilo.

Hali ya hewa hapa ni nyuzi joto 27 ambayo ni rafiki sana kwa wale wanaotoka Jiji lenye joto kali Dar es Salaam.Ninayo mengi ya kuandika kuhusu Hale lakini acha niiishie hapa maana vidole vimeshachoka kuandika hasa ukizingatia umri wangu mkubwa nilionao.Tukutane Hale Lounge.

Kionambali M.Kionambali

P.O.BOX 2785

0754-629298

Kisiju/Mkuranga/Pwani

Post a Comment

0 Comments