DK.MWINYI KUENDELEZA UJENZI WA SKULI ZA GHOROFA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea na utekelezaji wa mkakati wa ujenzi wa skuli za ghorofa kama suluhisho la kudumu la changamoto ya uhaba wa madarasa na uendeshaji wa skuli kwa zamu ya asubuhi na mchana.
Ameeleza kuwa lengo la Serikali ni kuongeza bajeti ya sekta ya elimu hadi kufikia Shilingi Trilioni Moja na kuifanya sekta hiyo kuwa sekta mama ya kipaumbele kwa maendeleo ya nchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipoifungua Skuli Mpya ya Msingi ya Muungano iliyopo Kibanda Maiti, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amefahamisha kuwa katika utekelezaji wa mkakati huo, tayari Serikali imeshasaini mkataba na Benki ya CRDB wenye thamani ya Shilingi Bilioni 240 kwa ajili ya ujenzi wa skuli 29 za ghorofa, na kwamba maandalizi ya ujenzi huo tayari yameanza katika maeneo ya Fuoni Kibondeni, Jumbi na Chunga kwa Unguja, pamoja na Kiuyu Minungwini, Mchanga Mdogo na Micheweni kwa Pemba kupitia mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Aidha, amesema kuwa mapema mwaka 2026 Serikali itaanza ujenzi wa skuli za ghorofa katika maeneo ya Jang’ombe, Mikunguni, Kianga na Mtoni Kidatu kwa Unguja, pamoja na Kengeja, Wesha na Miti Ulaya kwa Pemba, ambapo kwa kutumia fedha za Serikali itajenga skuli 18 za ghorofa Unguja na Pemba.
Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Nane tayari imejenga skuli 35 za ghorofa, hatua iliyopunguza changamoto ya mlundikano wa wanafunzi madarasani. Hata hivyo, amesema bado yapo maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya mlundikano wa wanafunzi na uendeshaji wa mfumo wa zamu, hususan Mkoa wa Mjini Magharibi ambao una nusu ya wakaazi wote wa Zanzibar.
Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa Zanzibar ni visiwa vyenye eneo dogo la ardhi na kwa kuzingatia kasi ya ongezeko la idadi ya watu linalofikia wastani wa asilimia 3.7 kwa mwaka, ni lazima kutumia busara katika matumizi ya ardhi iliyopo.
Ameeleza kuwa uimarishaji wa miundombinu ya elimu si suala la hiari bali ni la lazima ili kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya mazingira bora ya kujifunzia.
Akizungumzia ujenzi wa Skuli ya Muungano, amesema una maana kubwa katika historia ya misingi ya Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliolenga kubadili maisha ya wananchi wa Zanzibar kwa kuweka mbele haki, usawa na upatikanaji wa huduma za msingi ikiwemo elimu.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inaendelea kulinda misingi ya Mapinduzi kwa kuhakikisha watoto wote wanapata fursa sawa ya elimu bora ili kujenga kizazi chenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kuendeleza Taifa lao.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika sekta ya elimu, na katika mwaka wa fedha 2025/2026 imepanga kuziunganisha skuli 70 na mkongo wa mawasiliano pamoja na kuzipatia skuli kompyuta za mezani 2,000 kwa ajili ya maabara, kompyuta mpakato 4,000 pamoja na kuanzisha Madarasa Janja 25 (Smart Classroom) kwa lengo la kuongeza ufanisi wa ufundishaji na kujifunzia.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inatambua kuwa kasi ya ujenzi wa skuli mpya na upanuzi wa fursa za elimu unahitaji pia uwekezaji wa kutosha katika rasilimali watu, hususan walimu, ambapo katika mwaka 2024/2025 imeajiri walimu wapya 1,741 ili kukidhi mahitaji ya skuli mpya.
Aidha, amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali imeendelea na ajira na tayari imeajiri walimu wapya 492, huku lengo likiwa ni kuajiri walimu 1,500 pamoja na kuimarisha maslahi yao.
Akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu ujenzi wa Skuli ya Muungano, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Ndg. Khamis Abdalla Said, amesema skuli hiyo yenye ghorofa tatu ina jumla ya madarasa 42, maabara, chumba cha TEHAMA, vyoo 52 pamoja na maktaba. Ameeleza kuwa skuli hiyo imejengwa na Kampuni ya FUCHS Construction kwa gharama ya Shilingi Bilioni 6.1 na ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,890 kwa wakati mmoja kwa wastani wa wanafunzi 45 kwa kila darasa.


0 Comments