Mgombea Ubunge wa Jimbo la Babati Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, amekamilisha rasmi ziara yake ya kampeni ya siku 58 kwa kutembelea kata zote 25 za Jimbo hilo, akiwahimiza wananchi kupiga kura za ndiyo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Licha ya kutokuwa na mpinzani katika kinyang’anyiro cha ubunge, Sillo amesema aliona umuhimu wa kuwafikia wananchi katika maeneo yote ya Jimbo hilo ili kuomba kura za CCM kuanzia ngazi ya Urais, ambapo mgombea ni Dkt. Samia Suluhu Hassan, hadi ngazi ya Udiwani.
Akizungumza katika mkutano wa kufunga kampeni uliofanyika kata ya Kiru, Sillo alisema wananchi wa Babati Vijijini wamemhakikishia ushindi wa kishindo kwa CCM kutokana na kazi kubwa iliyotekelezwa na serikali katika kipindi cha miaka iliyopita.
“Nimepita kata zote 25, wananchi wameonyesha imani kubwa kwa CCM na wameniambia kura zao zote ni za ndiyo kwa Dkt. Samia, kwa mimi, na kwa madiwani wetu. Hii ni ishara kwamba wananchi wameona matunda ya maendeleo,” alisema Sillo.
Sillo aliendelea kuwanadi wagombea wa CCM kwa kuahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, umeme katika vitongoji vyote, ujenzi wa barabara, na madaraja yanayounganisha vijiji na kata mbalimbali.
Amesema dhamira ya serikali ya CCM ni kuhakikisha kila kijiji ndani ya Jimbo hilo kinakuwa na huduma bora za kijamii, akisisitiza kuwa maendeleo hayo yatawezekana endapo wananchi wataendelea kuiamini na kuiunga mkono CCM.
“Kura ya ndiyo kwa CCM ni kura ya maendeleo, amani na utulivu. Tumejipanga kuhakikisha huduma zote muhimu zinawafikia wananchi wa Babati Vijijini bila ubaguzi,” aliongeza Sillo.
Mkutano huo wa kufunga kampeni ulihudhuriwa na mamia ya wananchi, viongozi wa CCM ngazi mbalimbali, na makada wa chama waliokuwa wakihamasisha amani, umoja na mshikamano kuelekea uchaguzi.


.jpeg)

.jpeg)