Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi kimesema hakitishiki wala kustushwa na mbwembwe za upinzani kwa kuwa kina uhakika wa kupata ushindi mnono kupitia masanduku ya kura ifikapo oktoba 29 Mwaka huu.
Katibu wa Kamati Maalum vya NEC Zanzibar , Idara ya Itikadi ,Uenezi na Mafunzo , Khamis Mbeto Khamis ameeleza hayo huku akithibitisha mgombea Urais wa CCM Rais Dk Huseein Ali Mwinyi atarudi ikulu kwa kishindo .
Mbeto alisema kuna mambo matano muhimu yaliofanyika katika miaka mitano ya uongozi wa Rais Dk Mwinyi yatakayomfanya arudi tena ikulu kwa ridhaa ya Wananchi.
Akiyataja masuala hayo, alisema ni kuitikiwa kwake na wananachi wa makundi yote ,utawala wake kupinga vitendo vya ubaguzi , msisimko wa maendeleo ya aina yake ,huku akitimiza ahadi za chama na zake binafsi .
"Zanzibar ya sasa sio ile ilioachwa na wakoloni .Rais Dk Mwinyi ameendeleza kazi ilioanzishwa na watangulizi wake. Amezishughulikia changamoto za msingi na kuzipatia majibu ya kudumu "Alisema Mbeto
Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisema kutokana na uchapakazi wake miaka mitano iliopita,kura za ushindi wa Rais huyo hazina shaka hivyo nguvu ya umma itamrudisha tena madarakani .
"Hivi sasa Zanzibar hazitajwi changamoto katika sekta ya elimu, uhaba wa madawati na madarasa.Sasa kuna masoko bora ,barabara za lami , zahanati na hospitali zenye tiba na dawa "Alieleza
Mbeto akizungumzia uwajibikaji,utendaji na uwazi katika Serikali, alisema yamefanyika mageuzi makubwa ya kimfumo pamoja na umakini katika ukusanyaji wa mapato ya serikali .
Pia kazi nyingine ambayo itaongeza mtaji wa kura za Rais ni ukarabati mkubwa katika viwanja vya ndege , ujenzi wa Bandari, na kuanza mchakato wa Uchimbaji wa Mafuta na gesi .
"Uongozi wa Rais Dk Mwinyi umewaunganisha wananchi na kuwa jamii moja .Hakuna malalamiko ya upendeleo maeneo ya kazi. Kila mtumishi huwajibika kwa nafasi yake" Alisema Katibu huyo Mwenezi.
Tags
Habari
