Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasisitiza Watumishi wa Umma kuendelea kufanya kazi kwa uzalendo na uwajibikaji, wakizingatia misingi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Amesema lengo la Serikali ni kuimarisha zaidi maslahi ya Watumishi wa Umma hapa nchini kulingana na ukuaji wa uchumi, na kwamba Serikali imedhamiria kufikia asilimia 10 kutoka ukuaji wa sasa wa asilimia 7.4.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 25 Oktoba 2025, alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Umma katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa mageuzi na mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika sekta ya Utumishi wa Umma katika kipindi cha miaka mitano iliyopita yameonesha dhamira ya kweli ya Serikali ya kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha wanapata huduma bora na kwa wakati.
Amesema kuwa katika kipindi hicho, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha Utumishi wa Umma, ikiwemo kuboresha mazingira ya kazi, kuongeza mishahara, posho na pensheni kwa wastaafu.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imejipanga kuimarisha mifumo ya kidijitali kwa dhamira ya kurahisisha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na kupunguza urasimu katika taasisi za umma.
Aidha, amefahamisha kuwa Serikali imeanzisha mifumo mbalimbali ambayo tayari imeleta ufanisi mkubwa, ikiwemo Mfumo wa Taarifa za Watumishi na Malipo (HCMIS), ambao umeleta mageuzi makubwa katika usimamizi wa rasilimali watu na malipo ya watumishi.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa Watumishi wa Umma kuwa tayari kuipokea na kuitumia mifumo hiyo ili kuongeza ufanisi. Amebainisha kuwa katika kipindi cha kwanza cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane, Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza malalamiko na changamoto katika sekta ya utumishi.
Ameeleza kuwa Serikali imeweka mifumo inayozingatia kiwango cha elimu, uzoefu na muda wa ajira, hatua ambayo imechangia kuongeza ari ya watumishi katika kuwatumikia wananchi.
Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa Serikali imewapatia mafunzo watumishi 1,519 waliopata fursa za mafunzo ya muda mrefu ndani ya nchi, watumishi 65 waliopata mafunzo ya muda mrefu nje ya nchi, na wengine 631 waliopata mafunzo ya muda mfupi nje ya nchi.
Rais Dkt. Mwinyi amesema lengo la Serikali ni kuwa na kizazi kipya cha Watumishi wa Umma wenye maarifa, ujuzi na mitazamo mya inayolenga katika kuimarisha utumishi na maendeleo ya taifa.
Naye, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi ifikapo tarehe 29 Oktoba kupiga kura na kumchagua kiongozi mwenye maono ya kuendeleza maendeleo nchini.

.jpeg)


