Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Bw. Lazaro Twange amefanya
ziara ya kuagua maendeleo ya Miradi ya umeme ukiwemo wa Njia ya
kusafirisha umeme kutoka Zuzu hadi Mbande, Mradi wa kusambaza umeme
ardhini katika mji Serikali na Mradi wa Kituo cha kupokea na kupoza
umeme cha Mjini Mkoani Dodoma.
Bw. Twange ameelezea maendeleo ya
Mradi wa njia ya kusambaza umeme wa Msongo wa Kilovolti 33 kutoka Mbande
hadi Zuzu kwamba umefikia asilimia 48.35 huku Mradi wa usambazaji wa
umeme ardhini kwenye mji wa Serikali Ihumwa ukifikia asilimia 64 ambapo
hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 50.09 ambapo
amewataka Wakandarasi kuongeza kasi ili Miradi hiyo ikamilike kwa wakati
na ianze kuwahudumia wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji huyo pia
amekagua maendeleo ya Mradi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha
Mjini Dodoma ambacho kimefikia zaidi ya asilimia 80 na kinatarajia
kukamilika rasmi mwanzoni mwa mwezi Septemba Mwaka huu.
‘’Kituo
cha kupokea umeme cha mjini kimefikia zaidi ya asilimia 80, nataka
kuwaeleza kuwa mwanzoni mwa mwezi wa tisa Kituo hiki kitakamilika.Kituo
hiki kitatupa uwezo wa kuwasambazia umeme wateja wetu walioko Katikati
ya mji kwa kuwa kituo kilichokuwepo awali kilizidiwa na tunachotaka ni
kumudu mahitaji ya wateja wetu, alifafanua Bw. Twange.
Aidha,
Bw.Twange amesema licha ya changamoto za kifedha zilizojitokeza kwa
baadhi ya miradi amewapongeza wasimamizi wa Miradi kutoka TANESCO na
Wakandarasi ambapo ameeleza kuwa kukamailika kwa miradi hiyo kutachangia
upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma na
maeneo Jirani ya Mkoa wa Morogoro.
0 Comments