Afisa Ustawi
wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi. Amina Mfaki amezitaka
Halmashauri za Wilaya ya Chamwino, Halmashauri ya Wilaya Manyoni na
Halmashauri ya Wilaya ya Singida kuweka mikakati thabiti ya kuendelea
kulea kaya na vikundi mbalimbali vilivyokuwa vikisimamiwa kupitia Mradi
wa kusaidia Kaya Masikini na kaya zenye watu wenye ulemavu kutoka
shirika la BRAC Maendeleo ambao umefika mwisho.

Bi. Amina
ameyasema hayo Katika kikao cha kufunga Mradi wa kusaidia kaya Masikini
na kaya zenye watu wenye ulemavu kutoka shirika la BRAC Maendeleo
ambao umekuwa ukihudumia watu wenye ulemavu na Kaya zisizo na uwezo
katika Halmashauri hizo Wilayani Chamwino, mkoani Dodoma.
“Tumeona
namna gani wameweza kuwainua watu wa Kaya zisizo na uwezo na watu wenye
ulemavu, hivyo tunatarajia baada ya BRAC Maendeleo kumaliza muda wao ni
jukumu la Halmashauri zote kuendelea kusimamia zile kaya na watu wote
ambao walikuwa ni wanufaika wa Mradi"
Naye, Meneja wa Mradi wa
kusaidia kaya masikini na kaya zenye watu wenye ulemavu kutoka shirika
la BRAC Maendeleo Bi. Rachel Bwiliza ameishukuru Serikali kupitia Ofisi
ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ushirikiano mkubwa katika kufanikisha
mradi huo.
Amesema mradi huo umetekelezwa Kwa kipindi cha miezi
30 na umekekezwa katika Mikoa ya Dodoma na Singida katika Halmashauri
tatu na kufanikiwa kuwahudumia wahitaji zaidi ya 1,050 ambapo 85% kati
ya hao ni kaya zinazoongozwa na wanawake wenye kipato cha hali ya chini
huku 15% ikiwa ni kaya za watu wenye ulemavu.