Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mkazo katika
kulinda na kudumisha amani nchini ili kuhamasisha maendeleo na kuziba
mianya ya kuibuka kwa migogoro miongoni mwa wanajamii.
Ametoa
kauli hiyo leo Jumapili Juni 29, 2025 wakati alipomwakilisha Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kufunga kongamano la Afrika Mashariki la Amani
lililoandaliwa na The Islamic Foundation, katika viwanja vya shule ya
msingi Mirongo jijini Mwanza
“Nataka niwaambie bila amani
hatuwezi kupata mafanikio yoyote, kupitia kongamano hili mmepata nafasi
ya kujadili kuhusu tunu hii ya amani, ambayo wakati wote tumeshuhudia
viongozi wa dini mkiwa kwenye majukwaa yenu mkihimiza amani miongoni mwa
wanajamii, tuishike tunu hii”.
Kadhalika, amewataka Watanzania
kuangalia kwa upana wake suala la mmomonyoko wa maadili katika jamii
hasa kwa vijana. “Ni muhimu sana suala hili mkaliweka kama agenda katika
mikutano na vikao vyenu, kila kiongozi wa dini anapozungumza, suala la
maadili na mmomonyoko wa liwe ni ajenga ya kudumu”
Amesema kuwa
mabadiliko ya teknolojia na kuiga tamaduni za mataifa ya nje imekuwa
miongoni mwa chanzo kikubwa cha mmomonyoko wa maadili. “Siku hizi vijana
kuwaita wazee kwa majina yasiyo na heshima ni kitu cha kawaida,
viongozi ndio wenye jukumu la kusimamia eneo la maadili, mkifanya hivyo
tupata vijana wenye maadili mema”
Pia Mheshimiwa Majaliwa
amesema kuwa falsafa ya 4R ya Resilience (Ustahimilivu), Reconciliation
(Maridhiano) and Reforms (Mageuzi), Rebulding (Kujenga upya)
iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita katika misingi
imara ya kulinda amani. “Falsafa hii imeifanya Tanzania kuwa tulivu na
salama”
Wakati huo huo Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa jamii
inapaswa kuona umuhimu wa kukuza utamaduni wa majadiliano na maridhiano
katika kushughulikia tofauti zilizopo mingoni mwa jamii.
“Tunapaswa
kujenga jamii inayoheshimu maoni tofauti, na kuhimiza mijadala kwenye
majukwaa na kwa nafasi hii viongozi, taasisi na wanajamii mnapaswa kuwa
daraja la maridhiano badala ya kuwa vyanzo vya migawanyiko”
Naye
Mwenyekiti wa Islamic Foundation Aref Nahdi amesema kuwa taasisi zao
zitaendelea kushirikiana na Serikali katika kuijenga Tanzania.