Chama tawala
nchini Uganda, National Resistance Movement (NRM), kimethibitisha kuwa
Rais Yoweri Museveni atagombea muhula mwingine katika Uchaguzi Mkuu wa
2026 nchini humo.
Tangazo hilo linaweka mazingira kwa Museveni
kurefusha utawala wake wa takriban miongo minne nchini Uganda, nchi
ambayo inamfahamu mkuu mmoja tu wa serikali tangu Januari 1986. Kwa
sasa, Museveni ni kiongozi wa nne barani Afrika aliyetawala kwa muda
mrefu zaidi, huku chama tawala kikiwa kimefanyia marekebisho katiba ya
Uganda mara mbili huko nyuma ili kumruhusu kuongeza muda wa utawala
wake.
Mpinzani wa karibu wa Museveni atakuwa mwanasiasa Robert
Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, ambaye alishika nafasi ya pili katika
kura za mwisho za mwaka 2021 na tayari amethibitisha nia yake ya
kugombea 2026.
Wakati huo huo, kiongozi mwingine mkuu wa
upinzani na mpinzani wa muda mrefu wa Museveni, Dkt. Kizza Besigye, bado
yuko kizuizini baada ya kutekwa nyara mjini Nairobi tarehe 16 Novemba
2024 na kusafirishwa kurudi Uganda kupitia barabara.
Besigye anakabiliwa na mashtaka mengi yakiwemo ya kumiliki silaha na uhaini.