MAJALIWA ASEMA RAIS SAMIA AIMARISHA DIPLOMASIA YA UCHUMI

 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ametumia fursa ya hotuba ya kuhitimisha mkutano wa 19 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupongeza juhudi na mafanikio makubwa yaliyofanikishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha uhusiano wa kimataifa na diplomasia ya uchumi.

 Waziri Mkuu Majaliwa amesema, maono ya Rais Samia katika kuifungua Tanzania kiuchumi na kisiasa yameleta mafanikio makubwa kwa taifa, na kuiweka nchi katika nafasi ya heshima na ushawishi katika majukwaa ya kimataifa.

Katika hotuba hiyo, Waziri Mkuu ametaja mafanikio kadhaa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Dkt. Samia, ikiwa ni pamoja na ushiriki wa Tanzania katika mikutano ya kimataifa yenye umuhimu wa kiuchumi na kisiasa kama vile Mkutano wa Wakuu wa Nchi Tajiri Duniani (G20) uliofanyika Rio de Janeiro, Brazil na Mkutano wa COP 29 kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi. Ushiriki huu umeimarisha ushirikiano wa kimataifa na nafasi ya Tanzania duniani.

Aidha, Tanzania imeandaa mikutano mikubwa ya kimataifa ikiwemo Africa Energy Summit 2025 na Africa Food Systems Summit 2023, ambayo imetoa fursa kwa nchi kujitangaza kiuwekezaji, kubadilishana maarifa na kufungua milango ya ushirikiano mpya wa kimkakati.

Kupitia ziara za kimataifa na mapokezi ya viongozi wakuu kutoka nje ya nchi, Tanzania imeweza kusaini mikataba muhimu ya maendeleo. Miongoni mwa mafanikio hayo ni makubaliano kati ya Tanzania, Zambia na China ya kufufua reli ya kihistoria ya TAZARA, hatua inayotarajiwa kuboresha kwa kiwango kikubwa huduma za reli na uchumi wa ukanda huu.

Vilevile Waziri Mkuu amelieleza Bunge kuwa, Rais Samia pia amepokea rasmi Uenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC. Chini ya uongozi wake, Tanzania imesimamia kwa mafanikio uangalizi wa chaguzi katika nchi mbalimbali za Kusini mwa Afrika kama Botswana, Mauritius, Msumbiji na Namibia.

Post a Comment

0 Comments