RUTO ASEMA WACHINA HAWATAENDESHA BIASHARA ZA REJAREJA KENYA

Rais wa Kenya, William Ruto, ameagiza hatua za kiutawala zichukuliwe dhidi ya raia wa kigeni wanaojihusisha na biashara ndogo ndogo na uchuuzi nchini humo, akisisitiza kuwa Kenya haitaruhusu wageni kuingia na kutawala sekta ya biashara za rejareja.

Ruto amesema hatua hiyo inalenga kuwalinda wafanyabiashara Wakenya dhidi ya ushindani usio wa haki, hasa kutoka kwa raia wa kigeni wanaoingia katika biashara ndogo ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikifanywa na wananchi wa Kenya.
 
Akizungumza na wafanyabiashara kutoka sekta ya biashara ndogo, ndogo na za kati katika Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto amesema hatua dhidi ya wachuuzi wa kigeni zitaanza kuchukuliwa wiki ijayo.
 
Katika msimamo wake, Ruto amesisitiza kuwa Kenya haitakubali raia wa China kuendesha biashara za rejareja nchini, akieleza kuwa serikali yake inataka kuhakikisha Wakenya wanapata fursa ya kufanya biashara na kujenga uchumi wao.
 
Aidha, Rais Ruto amefichua kuwa kuna Muswada unaoshughulikiwa na Bunge ambao unapendekeza kuweka vikwazo kwa raia wa kigeni kufanya baadhi ya shughuli za biashara nchini Kenya.
 
Rais huyo pia ameiagiza Wizara ya Uhamiaji kuchunguza na kufuatilia masharti yanayotumika kuwapatia wawekezaji wa kigeni vibali vya kufanya biashara nchini humo.
 
Hatua hizo zinatarajiwa kuibua mjadala kuhusu namna Kenya inavyoweza kulinda wafanyabiashara wake wa ndani, huku ikiendelea kuvutia uwekezaji wa kigeni unaochangia ukuaji wa uchumi.

Post a Comment

0 Comments