Takribani
watu 30 wamefariki dunia na wengine 22 kujeruhiwa baada ya mlima wa taka
kuporomoka na kuangukia nyumba zilizokuwa karibu katika mji mkuu wa
Guinea, Conakry, kufuatia mvua kubwa kunyesha.
Tukio hilo
limetokea majira ya saa nane usiku katika eneo la Dar es Salaam jijini
Conakry. Serikali ya Guinea imesema dampo hilo liliporomoka ghafla baada
ya mvua kubwa, huku ikihofiwa kuwa watu kadhaa wamekwama chini ya
vifusi.
Serikali imetuma idadi kubwa ya vikosi vya usalama, ikiwemo jeshi, kushiriki katika shughuli za uokoaji.
Akizungumza na vyombo vya habari vya ndani, mwanamke mmoja amesema watoto wake watano wamefariki katika tukio hilo.
Mamlaka
zinaendelea na shughuli za uokoaji, huku zikihofia kuwa watu zaidi
huenda wamefunikwa na vifusi na hivyo idadi ya vifo ikaongezeka.
Waziri Mkuu wa Guinea, Amadou Ouari Ba, ametembelea eneo la tukio na kutathmini hali ilivyo.
Awali,
kiongozi wa eneo hilo, Lansine Sila, aliliambia shirika la habari la
AFP kuwa kulikuwa na hofu ya idadi kubwa ya waathiriwa. Amesema hadi
wakati huo miili 18 ilikuwa imepatikana na kupelekwa katika chumba cha
kuhifadhia maiti.
0 Comments