Watu kadhaa wanahofiwa kufariki dunia na wengine kujeruhiwa katika ajali ya basi la abiria iliyotokea leo katika eneo la Ngukumo, Kata ya Nkiniziwa, Wilaya ya Nzega, Mkoa wa Tabora.
Ajali hiyo imehusisha basi lenye namba za usajili T.840 EAS, mali ya Kampuni ya Miza Express, ambalo limeacha njia na kupinduka wakati likiwa safarini.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa ajali hiyo imesababisha hali ya taharuki katika eneo hilo, huku idadi kamili ya waliofariki na kujeruhiwa bado haijathibitishwa rasmi.
Mara baada ya tukio hilo, shughuli za uokoaji zimeanza kufanyika chini ya uratibu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na wananchi waliofika eneo la ajali kusaidia waathirika.
Waokoaji wanaendelea na zoezi la kuwatoa abiria waliokwama ndani ya basi, huku majeruhi wakitarajiwa kupelekwa katika vituo vya afya kwa ajili ya kupata matibabu.
Mamlaka husika zinaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo, pamoja na kuthibitisha idadi kamili ya waliofariki na kujeruhiwa.
.jpeg)
0 Comments