Jeshi la
Polisi Mkoa wa Rukwa linawashikilia watu 29 kwa tuhuma za kuhusika na
tukio la Mauaji lililotokea katika Kijiji cha Madibila, Wilaya ya
Kalambo mkoani Rukwa, baada ya kuzuka kwa vurugu zilizodaiwa kuchochewa
na taarifa za uongo kuhusu kuibiwa kwa Nyeti.
Kwa mujibu wa
taarifa ya Jeshi la Polisi, tukio hilo lilitokea Agosti 20, 2026, majira
ya saa 12:45 jioni, baada ya Vijana saba kufika kijijini hapo kwa ajili
ya kutoa huduma za usajili wa laini za simu.
Wakati wakiendelea
na shughuli hiyo, kulitokea taharuki baada ya Mwananchi mmoja aitwaye
Mpaji Simkanji kudai kuwa alikuwa ameibiwa Nyeti zake. Madai hayo
yalisababisha baadhi ya Wananchi kuanza kuwashambulia vijana hao kwa
kutumia mawe, fimbo na silaha nyingine za jadi.
Katika vurugu
hizo, kijana mmoja, Devid Amos Mwimanz, mwenye umri wa miaka 22, mkazi
wa Kijiji cha Kasanga, aliuawa na wenzake wengine kujeruhiwa maeneo
mbalimbali ya miili.
Polisi pia imesema wananchi hao walichoma
moto gari aina ya Nissan lenye namba za usajili T.157 DQP, lililokuwa
likitumiwa na vijana hao kwa usafiri.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini hatua zaidi za kisheria dhidi ya watuhumiwa hao.
Aidha,
Jeshi hilo limetoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuendekeza imani
za kishirikina na kujichukulia sheria mkononi, likieleza kuwa vitendo
hivyo vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii.
0 Comments