RAIS SAMIA:UMEME UTAMFIKIA KILA MWANANCHI

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewakosoa wanaodai kuwa Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) ni “white elephant” na kwamba hauna tija kwa Taifa, akisisitiza kuwa ujenzi wa njia kuu za kusafirisha umeme unaendelea kwa kasi kubwa ili kuhakikisha umeme unaozalishwa unafikishwa kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza Jumamosi, Agosti 22, 2026, Mkoani Pwani mara baada ya kuzindua mradi huo, Rais Samia alisema Tanzania inaendelea kuvutia uwekezaji, jambo linaloongeza mahitaji ya umeme kwa kasi. Alisema akiba ya umeme iliyopo sasa inaweza isiwe ya kutosha katika miaka michache ijayo, hivyo Serikali inaendelea kuwekeza katika vyanzo vingine vya nishati ikiwemo jua na upepo.


Rais Samia alisema madai kwamba mradi huo ni “tembo mweupe” hayana msingi, akieleza kuwa changamoto iliyokuwepo ya miundombinu ya kusafirisha umeme inashughulikiwa kwa kasi. “Ujenzi wa njia za kusafirisha umeme unaendelea kwa kasi kubwa na mradi huu ni mradi wa manufaa makubwa kwa Taifa na si kama wanavyosema,” alisema.


Aidha, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu kwa kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji vinavyoupa uhai, akiilekeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuratibu na kusimamia kwa karibu uhifadhi wa mazingira na vyanzo vyote vya maji, hususan vile vinavyohusiana na mradi huo.


Alisema jukumu la kulinda mazingira na vyanzo vya maji ni la kila mmoja, akisisitiza kuwa hatua hizo ni muhimu ili kuhakikisha Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere linaendelea kutoa manufaa kwa Taifa kwa miaka mingi ijayo.


 

Post a Comment

0 Comments