Upande wa
mashtaka unaoongozwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) umeitaka
mahakama Kuu kutowaita baadhi ya mashahidi waliotajwa na mshtakiwa Tundu
Lissu Mwenyekiti wa CHADEMA katika kesi ya uhaini inayomkabili.

Baada
ya mahakama kumkuta Lissu na kesi ya kujibu, Mwenyekiti huyo alitoa
orodha ya mashahidi kumi na mmoja ambao ameiomba mahakama iwaite kwa
ajili ya kutoa ushahidi katika kesi hiyo.
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka imesema mashahidi namba 1 hadi 7 wasiruhusiwe kuja kutoa ushahidi.
Mashahidi
ambao DPP imetaka wasiitwe ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan,
Makamu wa Rais, Philip Mpango, pamoja na Kassim Majaliwa aliyekuwa
Waziri Mkuu.
Wa nne ni Camillus Wambura, Mkuu wa Jeshi la Polisi
Tanzania. Wa tano ni Jenerali John Mkunda, Mkuu wa Majeshi Tanzania.
Shahidi wa sita ni Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS).
Shahidi wa saba ni Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Kanali wa Polisi
Ramadhani Kindai.
Kuhusu mashahidi watatu wa awali, waendesha
mashtaka wamesema hao ni viongozi wa serikali inayomtuhumu Lissu kwa
kosa la kutishia Katiba ya nchi.
DPP imeiomba mahakama iuone
ushahidi wa mashahidi hawa saba kuwa si muhimu kwa sababu ushahidi wao
umeshatolewa na mashahidi wa upande wa serikali ambao ni watumishi wa
serikali.
0 Comments