DKT:TUENDELEE KULIOMBEA TAIFA NA KUDUMISHA AMANI

Waziri, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kuendelea kuliombea Taifa na kudumisha amani, akisema amani ni msingi unaowezesha wananchi, taasisi za dini na Taifa kwa ujumla kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.

Amesema dunia inaendelea kushuhudia mabadiliko na mitikisiko katika maeneo mbalimbali, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kumwomba Mungu ailinde Tanzania na kuendeleza amani ambayo imeiwezesha nchi kutekeleza shughuli zake kwa utulivu.


Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumapili, Agosti 23, 2026) aliposhiriki ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Usharika wa Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

“Tuendelee kuiombea nchi yetu. Leo hii tunaweza kufanya ibada kwa sababu nchi yetu ipo na amani. Tuna mipango mbalimbali kama nchi, katika ngazi ya familia, taasisi, Dayosisi na Kanisa, lakini hayo yote tunaweza kuyafanya kama nchi yetu ipo na amani,” amesema.

Dkt. Mwigulu amewafikishia waumini salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Serikali kwa ujumla, huku akitambua na kuenzi mchango mkubwa unaofanywa na Kanisa katika maendeleo ya nchi.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kusonga mbele.

“Hauwezi ukataja maendeleo ya nchi yetu bila kutaja mchango wa Kanisa,” amesema.


Post a Comment

0 Comments