SERIKALI YAWEKEZA BILIONI 7 KUSAMBAZA UMEME MIGODINI NCHINI

 Wachimbaji wadogo wa madini wilayani Nyang’hwale, mkoani Geita, wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika upatikanaji wa nishati ya umeme kwenye maeneo ya migodi, hatua inayopunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija katika shughuli za uchimbaji.

Shukrani hizo zimetolewa wakati nilipozindua mradi wa kuzalisha nishati ya umeme wenye uwezo wa KVA 500 kwenye Mgodi wa wachimbaji wadogo katika eneo la Igalula, wilayani Nyang’hwale. Mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 426 na ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya nishati katika maeneo ya uchimbaji wa madini.

Serikali imeendelea kutekeleza kwa vitendo dhamira ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na uzalishaji katika sekta ya madini kwa kusambaza umeme kwenye migodi ya wachimbaji wadogo na wa kati.

Serikali tayari imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 7 kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ya migodi nchini, hatua iliyowezesha wachimbaji kupunguza utegemezi wa mitambo inayotumia mafuta na hivyo kushusha gharama za uzalishaji huku ikiongeza ufanisi wa shughuli za uchimbaji.

Nilikagua pia mradi wa maji safi na salama unaotekelezwa katika Kijiji cha Kakola, ambao unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wananchi 24,801

Nimezindua pia Shule ya Msingi na awali ya Imara Baruti iliyojengwa ili kuondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali wa takribani kilomita nne kwenda kusoma katika Shule ya Msingi Shabaka.

Serikali ya chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuthibitisha kuwa ahadi zinazotolewa kwa wananchi si maneno ya kampeni pekee, bali ni mipango inayotekelezwa kwa vitendo kwa manufaa ya Watanzania.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, amempongeza Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kazi kubwa iliyofanyika ndani ya muda mfupi katika mkoa wa Geita ambayo imegusa sekta za Afya,Elimu,Nishati na Miundombinu huku akisema hatua hiyo imeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kuimarisha huduma zinazowagusa wananchi moja kwa moja.


 

Post a Comment

0 Comments