Hatimaye Rais
wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amesaini kuwa sheria muswada unaoongeza
muda wa urais kwa miaka miwili, hatua inayomruhusu kuendelea kuhudumu
madarakani hadi mwaka 2030.
Msemaji wa Serikali ya Zimbabwe, Nick
Mangwana, alithibitisha hatua hiyo, jana Jumanne Julai 7, 2026 kupitia
ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, akisema: "Imesainiwa,
imethibitishwa na sasa ni sheria," huku akiambatanisha nakala ya sheria
hiyo.
Mwezi uliopita, mabunge yote mawili ya Zimbabwe yaliidhinisha muswada huo baada ya mjadala mkali ulioibua maoni yanayokinzana.
Wanaounga
mkono hatua hiyo wanasema marekebisho hayo yatasaidia kupunguza gharama
za kuandaa uchaguzi, huku wanaoupinga wakidai yanadhoofisha misingi ya
demokrasia kwa kuwanyima wananchi haki ya kumchagua rais wao kupitia
kura ya moja kwa moja.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na
Idhaa ya Kiswahili BBC, sheria hiyo pia ina kipengele kinachoruhusu rais
kuchaguliwa na Bunge badala ya wananchi kumpigia kura moja kwa moja.
0 Comments