Na Moshi saidi.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutenga fedha kupitia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi la urasimishaji wa ardhi, hatua ambayo amesema itasaidia kutatua changamoto za migogoro ya ardhi zinazowakabili wananchi wa jiji hilo.
Mhe. Mpogolo amesema hayo Julai 22, 2026, baada ya kukutana na wananchi wa Kata ya Zingiziwa kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali, hususan migogoro ya ardhi. Katika kikao hicho, wananchi zaidi ya 26 walipata fursa ya kuwasilisha changamoto zao na kusikilizwa.
Amesema migogoro mingi ya ardhi inatokana na matumizi ya mifumo isiyo rasmi na ya kizamani katika kuuza na kununua ardhi, badala ya kufuata taratibu zinazotambuliwa na Serikali. Hivyo, amewahimiza wananchi kufika katika ofisi husika za Serikali ili kupata huduma na ushauri sahihi kabla ya kufanya miamala ya ardhi.
"Nawaasa muwe makini mnapotaka kununua au kuuza ardhi. Hakikisheni mnamtambua mmiliki halali wa eneo husika ili kuepuka utapeli. Tumekuja kusikiliza na kutatua changamoto zenu kwa kufuata maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi," amesema Mhe. Mpogolo.
Aidha, amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuepuka tamaa ya fedha wanapowahudumia wananchi, akisisitiza kuwa haki itendeke kwa kila mmoja bila upendeleo.
Vilevile, amewataka wamiliki wa mashamba na viwanja kuacha kuyaacha bila matumizi kwa muda mrefu, akieleza kuwa hali hiyo huchochea uvamizi na migogoro ya umiliki wa ardhi. Amesisitiza umuhimu wa kuyatunza na kuyasimamia mali hizo ili kulinda haki za wamiliki na kudumisha utulivu katika jamii.






0 Comments