SILLO AFANIKISHA HARAMBEE YA VYOMBO VYA MUZIKI QAMEYU, ZAIDI YA MILIONI 8 ZAKUSANYWA

 Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daniel Sillo ameongoza harambee ya ununuzi wa vifaa vya muziki kwa Kwaya ya Watakatifu Yoakimu na Anna ya Kanisa Katoliki la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Parokia ya Qameyu Jimbo la Mbulu.

Harambee hiyo ilienda sambamba na uzinduzi wa albamu yenye nyimbo tano ya kwaya hiyo iitwayo “Shangwe Zimetanda”, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na serikali pamoja na madiwani wa viti maalum wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati.

Katika risala iliyosomwa na Katibu wa Kwaya hiyo, Emmanuel Fissoo, wanakwaya hao wamesema wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya uinjilishaji katika maeneo mbalimbali kupitia huduma ya uimbaji, lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vyombo vya muziki.

Amesema ili kutatua changamoto hiyo, kwaya hiyo inahitaji kiasi cha shilingi milioni 8 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa muhimu vya muziki vitakavyosaidia kuboresha huduma yao ya uinjilishaji.

Kwa mujibu wa taarifa ya harambee hiyo, jumla ya shilingi milioni 7,649,900 zilipatikana papo hapo huku ahadi zikifikia shilingi laki sita, na kufanya jumla ya fedha na ahadi kufikia shilingi milioni 8,249,900, kiasi kilichovuka lengo lililowekwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Paroko wa Parokia ya Qameyu, Joakim Baran amesema mafanikio ya harambee hiyo yametokana na juhudi za waumini pamoja na neema za Mungu na muitikio mkubwa wa watu waliojitokeza kusaidia.

Aidha, Paroko huyo amemshukuru mgeni rasmi Daniel Sillo pamoja na wageni wote waliohudhuria kwa kufanikisha harambee hiyo na kuonesha mshikamano mkubwa kwa kanisa.

“Tunawashukuru wote waliochangia na kushiriki. Kanisa linaendelea kuiombea serikali yetu pamoja na viongozi wake wakati wote,” amesema Paroko Baran.


 

Post a Comment

0 Comments