RC MTANDA:UHIFADHI WA ZIWA VICTORIA NI UHAI WA UCHUMI WA WATU MILIONI 40

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Mei 18, 2026 ameshiriki tukio la upandaji miti kwa ajili ya uhifadhi wa vyanzo vya maji katika Chanzo cha Maji cha Butimba kilichopo Jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya kuelekea maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Ziwa Victoria.

Akizungumza katika shughuli hiyo, Mhe. Mtanda amesema uhifadhi wa ziwa Victoria ni muhimu kutokana na mchango wake mkubwa katika shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo uvuvi, biashara, usafiri na upatikanaji wa maji kwa wananchi wa ukanda wa ziwa.

Amesema zaidi ya watu milioni 40 wanategemea ziwa hilo kujipatia kipato na kuendesha shughuli mbalimbali za maendeleo, hivyo ipo haja ya kuweka mikakati madhubuti ya kulinda mazingira na vyanzo vya maji ili kuhakikisha rasilimali hiyo inaendelea kuwa salama kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Mhe. Mtanda amepongeza Wilaya ya Nyamagana pamoja na wadau wa mazingira kwa juhudi zao za kuendelea kuhifadhi misitu na mazingira huku akisisitiza kuwa mazingira salama ni msingi wa maisha bora kwa jamii.

“Hatupandi miti kwa ajili yetu pekee bali kwa ajili ya vizazi vijavyo vinufaike kama sisi tunavyonufaika kupitia waliopanda zamani,” amesema Mhe. Mtanda.

Aidha amewahamasisha wananchi kuendelea kupanda miti katika vyanzo vya maji pamoja na maeneo yao ya makazi ili kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewakaribisha wananchi kushiriki maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria yatakayotanguliwa kwa siku mbili za mikutano katika ukumbi wa Malaika hoteli na Nyamhongolo Wilayani Ilemela Mei 21.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Bi. Rose Ambrose amesema Serikali inaendelea kuimarisha Mradi wa Maji Butimba unaohudumia zaidi ya wananchi laki nne, huku lengo likiwa kuongeza huduma kwa wananchi laki nane. 

Amebainisha pia mkakati wa wizara hiyo wa kupanda miti 10,000 kuzunguka maeneo ya mradi ambapo miti zaidi ya 6,000 tayari imepandwa na miti 2,000 imepandwa leo ikiwa ni mwendelezo wa kampeni ya uhifadhi wa mazingira.


Post a Comment

0 Comments