Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameitaka tume ya maendeleo ya Ushirika kuendelea kusimamia nidhamu na weledi kwa watendaji na viongozi ndani ya vyama vya ushirika mkoani humo ili kuleta tija kwenye kilimo na kusaidia kukuza sekta hiyo muhimu.
Ametoa agizo hilo leo tarehe 28 Mei, 2026 wakati akifungua Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika la Mkoa huo na kuwataka kuhakikisha ndani ya vyama hivyo kunakua na utulivu utakaosaidia kukuza uzalishaji na uchumi wa mkoa katika ngazi ya taifa.
Mhe. Mtanda amebainisha kuwa kilimo ni ajira na kila mmoja ana wajibu wa kulisaidia taifa katika kukuza sekta ya ajira kwa kuhakikisha anashiriki katika uchumi wa kijani kwa kulima mazao ya chakula na biashara ili kukuza kupato
Naye Mrajisi msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mwanza Bi. Hilda Boniphace amesema jumuiya hiyo inaendelea kuboresha shughuli za vyama vya ushirika ikiwemo uwajibikaji na utunzaji wa mali za chama hicho ili kuhakikisha taratibu na sheria za uendeshaji zinafuatwa na kufanikisha kuanzisha mifumo ya kidigitali.
Vilevile, amebainisha kuwa chama hicho mkoani Mwanza kimepata hati safi 83 huku zisizoridhisha zikiwa ni 4 tu na kwamba wana mikakati ya kuhakikisha AMCOS zote zinafuata miongozo ya kazi kwa kushirikiana na Chama kikuu cha Ushirika cha mkoa huo.
Akitoa taarifa ya Chama Kikuu cha Ushirikia Mwanza (Nyanza Cooperative Union) mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Leonard Lyabalima amesema chama hicho kipo mbioni kuanzisha Kituo cha zana za Kilimo ili wakulima wapate matrekta na kufanya kilimo cha kisasa.
Aidha, amefafanua kuwa chama hicho kwa kushirikiana na taasisi zingine wanaimarisha mfumo wa kidigiti wa stakabadhi za ghala kwa mazao ya Choroko na Dengu kwa wakulima ili kubakikisha mazao hayo yanaleta tija kwenye uchumi wa wananchi.
Vilevile, amebainisha kuwa pamoja na kwamba Pamba ndilo zao kuu mkoani Mwanza, chama hicho kinaendelea na taratibu za kuimarisha zao la kahawa kwa kulifanya kuwa mbadala kwa wakulima na kwamba mpaka sasa wananchi elfu 25 wamepatiwa miche wilayani Ukerewe.

.jpeg)
.jpeg)
0 Comments