Na Moshi saidi.
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Mkoa wa ilala imesema imefanikiwa kufuatilia matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya shilingi Bilioni 52 katika wilaya hiyo kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi 2026.
Kauli hiyo imetolewa hii leo na Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa ilala Moza kasubi wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo amesema Taasisi hiyo imeweza kusaidia mradi wa kituo cha polisi Bonyokwa wenye thamani ya shilingi milioni 406.6 kuendelea na utekelezaji baada ya kusaidia mkandarasi M/S Nyakire Investment Limited kulipwa kiasi cha shilingi milioni 181.9 alizokuwa akiidai Halmashauri ya jiji la Dar es salaam kwa kazi alizokuwa ameshazitekeleza, ambapo hapo awali mkandarasi huyo alishindwa kuendelea na kazi kutokana na ucheleweshaji wa malipo hayo.
Kasubi ameongeza kuwa pia wamefanikiwa katika utekelezaji wa miradi mingine 6 yenye thamani ya shilingi Bilioni 51.6 kuhakikisha maboresho yenye kukidhi viwango vinavyotakiwa yamefanyika baada ya kubainika mapungufu katika baadhi ya kazi zilizokuwa zinatekelezwa.
Aidha kasubi aligusia katika suala zima la uelimishaji umma ambapo amesema Takukuru ilala kwa kipindi husika wameendelea kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa makundi mbalimbali ya wananchi na kuwafikia zaidi ya wananchi 19,320 huku wakitumia njia mbalimbali zikiwemo semina kwa makundi mbalimbali pamoja na vipindi vya Redio na Televisheni.
Naibu mkuu huyo wa Takukuru ameongeza kuwa jumla ya klabu za wapinga rushwa 33 zilimaarishwa kupitia utoaji mada mbalimbali juu ya athari za rushwa, semina 28 zimetolewa kwa watumishi wa umma, vipindi vya redio na televisheni 4 lengo likiwa ni kuwajengea uwezo kuelewa athari za rushwa na kuwajibika kila mmoja kwa nafasi yake kwa uadilifu.
Katika hatua nyingine Kasubi amesema Taasisi hiyo mkoani humo imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi milioni 57 iliyotokana na kesi ya uhujumu uchumi iliyohusisha washitakiwa wanne kwa makosa ya ubadhirifu na ufujaji, matumizi mabaya ya madaraka na kusaidia kutenda kosa ambapo washtakiwa hao walifanya ubadhirifu huo ikiwa ni mali ya chama cha wafanyakazi wa serikali za mitaa TALGWU huku washitakiwa hao wakirejesha shilingi milioni 57.5 katika akaunti ya Mkurugenzi wa mashtaka DPP iliyopo Benki kuu na kiasi kilichobaki kitakamilishwa katika awamu ya pili kwa mujibu wa makubaliano.

0 Comments