Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo kwa lengo la kuijenga nchi na kuimarisha maisha bora kwa wananchi.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 16 Mei 2026, alipokutana na Baraza la Wazee wa Afisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar katika mkutano maalum wa kutoa shukrani baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2026, uliofanyika Ikulu Zanzibar.
Amesema kazi kubwa iliyopo sasa ni kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya CCM unafanyika kwa vitendo ili malengo yote yaliyopangwa yawe yamekamilika ifikapo mwaka 2030.
Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba za kisasa kwa ajili ya makaazi ya wananchi, kwa lengo la kuwaondoa katika majengo chakavu yaliyojengwa zaidi ya miaka 60 iliyopita ambayo hayana usalama tena.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo afya, elimu, miundombinu, mawasiliano, bandari, barabara, viwanja vya ndege pamoja na nyumba za maendeleo za kisasa.
Akizungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Dkt. Mwinyi amesema majadiliano kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha ACT-Wazalendo yanaendelea vizuri huku yakizingatia maslahi ya Taifa, amani, mshikamano na umoja wa wananchi.
Amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Zanzibar inaendelea kuwa nchi yenye utulivu na kuondoa chuki miongoni mwa wananchi kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Taifa.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar, Ndg. Waziri Mbwana Ali, amesema Baraza hilo limempongeza Dkt. Mwinyi kwa kuimarisha umoja, amani na utulivu wa nchi pamoja na kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini.






0 Comments