MWANAMITINDO ATUMIA MIKATE 500 KUDESIGN GAUNI

Na Ally Mandai 

Usiku wa utoaji wa Tuzo za Africa Magic Viewers' Choice Awards (AMVCA) jijini Lagos uliibua gumzo kubwa kutokana na mitindo na ubunifu mbalimbali uliotawala kwenye zulia jekundu, huku mmoja wa waliovuta hisia za wengi akiwa ni mfanyabiashara na mwanamitandao maarufu Queen Mercy Atang.
 
Queen Mercy Atang aliwashangaza wengi baada ya kuonekana akiwa amevaa gauni kubwa lililoripotiwa kutengenezwa kwa kutumia takribani mikate 500. Muonekano huo wa kipekee uliwafanya wengi kuzungumzia ubunifu wake huku wengine wakibaki na mshangao kuhusu namna vazi hilo lilivyobuniwa.
 
Inaelezwa kuwa Queen, aliyepata umaarufu baada ya kushiriki msimu wa sita wa Big Brother Naija mwaka 2021, alitumia fursa hiyo kuitangaza biashara yake ya mikate na keki inayojulikana kama Swit Cakes & Desserts.
 
Akizungumza na BBC wakati wa hafla hiyo, Queen alisema aliona AMVCA kuwa sehemu sahihi zaidi ya kuitangaza biashara yake mbele ya hadhira kubwa. “Nilijiuliza ni wapi pazuri pa kuitangaza biashara yangu, ndipo nikagundua hakuna sehemu bora zaidi ya kufanya hivyo kama hapa AMVCA,” alisema Queen.
 
Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilimuonyesha Queen akitembea kwenye zulia jekundu huku wasaidizi wake wakimsaidia kubeba sehemu ya chini ya gauni hilo kubwa lililopambwa kwa mikate.
 
Baada ya mwonekano huo kusambaa, watu wengi mitandaoni walitoa maoni tofauti. Baadhi walimpongeza kwa ubunifu na mbinu yake ya kipekee ya kutangaza biashara, huku wengine wakikosoa matumizi ya chakula katika mavazi wakati dunia ikiendelea kukabiliwa na changamoto za uhaba wa chakula kwa watu wengi.
 
Pamoja na mijadala hiyo, Queen hakusita kumpongeza mbunifu wa gauni hilo, Toyin Lawani wa Tiannah's Empire, kwa kufanikisha wazo lake.
 
“Toyin, asante kwa ubunifu wako na kwa kusaidia kuitangaza brand yangu. Nilihitaji gauni ambalo lingeonyesha wazi kuwa nina biashara ya bakery, na umeweza kufanya hivyo. Mwanzoni nilikuwa na hofu, lakini uliendelea kunipa moyo hadi mwisho,” alisema Queen

 

Post a Comment

0 Comments