JAMAA ADAI KUIBIWA MKE NA MWENYEKITI WA KITONGOJI

Na Ally Mandai  

Mkazi wa Mtaa wa Chomete wilayani Tarime mkoani Mara, Sisiemu Lucas, amedai kukumbwa na tukio la kuondokewa na mke wake ambaye anamtuhumu kuondoka na Mwenyekiti wa Kitongoji hicho pamoja na baadhi ya mali zake na watoto wao wanne.  

Lucas alitoa malalamiko hayo mbele ya Katibu wa NEC wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, wakati wa kikao cha kusikiliza kero za wananchi kinachoendelea mkoani Mara.

Akieleza kilichotokea, Lucas amesema mbali na kuondoka na mke wake, mwenyekiti huyo anadaiwa kuondoka pia na baadhi ya bidhaa zilizokuwa dukani kwake pamoja na watoto wao wanne, jambo lililomsababishia maumivu na hasara kubwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele, amesema tayari serikali inalifahamu suala hilo na uchunguzi wa awali umebaini kuwepo kwa sintofahamu kuhusu mahari, ambapo wazazi wa mwanamke huyo wanadaiwa kupokea mahari kutoka kwa wanaume wawili tofauti.

Gowele ameongeza kuwa pia kuna madai dhidi ya Lucas kuhusu tuhuma za ukatili wa ndoa, ikiwemo kumpiga mkewe, huku akieleza kuwa suala hilo linaendelea kushughulikiwa na Jeshi la Polisi.

Naye Kihongosi amesema amelipokea sakata hilo na kumpa pole Lucas, akimtaka kuendelea kufuata sheria na taratibu ili haki iweze kupatikana. Ameeleza kuwa ana imani vyombo vya dola vitalifanyia kazi suala hilo kwa weledi huku akiahidi kuendelea kufuatilia mwenendo wake. 

TANGAZA NYIMBO YAKO,BIASHARA AU UNA HABARI YOYOTE WASILIANA NASI KWA NAMBA HII 0654414804. 


 

Post a Comment

0 Comments