MBETO:RAIS MWINYI AGOMA KUVUNJA KATIBA ILI ABAKI MADARAKANI ZANZIBAR

Na Mwandishi  Wetu, Zanzibar 

Chama Cha Mapinduzi kimepongeza  uamuzi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti  wa Baraza la Mapinduzi , Rais Dk Hussein  Ali Mwimyi  kwa  kushinda majaribu ya wapambe walioanza kumshinikiza avunje katiba  na  kuongeza muda wa kubaki  Madarakani Zanzibar.

CCM kimesema ni fedheha kwa wapambe na mashabiki walioanza kumshawishi kiongozi huyo abaki madarakani kinyume na Katiba ya CCM na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu  wa Kamati  Maalum  ya NEC  idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo,  Khamis Mbeto Khamis,  aliyesema huo ndio uamuzi na msimamo wa CCM. 

Mbeto alisema kwa mujibu wa Mila na  Utamaduni  wa CCM ,  na kwa matakwa ya Katiba  ya Zanzibar ya mwaka 1984  na katiba ya CCM ,Rais  atakaa Madarakani vipindi viwili vya Miaka kumi  na hatawania tena nafasi hiyo. 

Alisema matamshi yaliotamkwa na baadhi ya wapambe kwa utashi wao binafsi, ulikuwa na dhamira  batili, kwani hakuna Rais  kupitia  CCM anayeweza  kupata nafasi ya kuongeza muda wa kubaki madarakani kinyume na taratibu. 

"Hata iweje kwa Rais aliye Madarakani  akitokea ameleta maajabu ya kiutendaji  katika kusimamia  maendeleo, muda wake  kikatiba utabaki kuwa ule ule wa miaka kumi madarakani .Kila Rais akimaliza miaka hiyo atawapisha  wengine. "Alisema Mbeto. 

Aidha ,Katibu huyo Mwenezi aliliita tangazo la Rais Dk  Mwinyi kukataa kubaki ikulu ifikapo mwaka 2030 , hana   fikra wala mpango  wa kuongeza muda ili abaki  madarakani ni aibu kwa walioanza kumshabikia.  

"Kiongozi  yeyote muungwana huheshimu Katiba aidha ya chama na katiba ya nchi. Kuvunja  ahadi na miadi au kufanya kinyume chake hiyo ni  dalili ya kiongozi huyo kukosa utu na ustaarabu" Alisisitiza.

Mbeto alisema Tanzania hususan ndani ya CCM, kuna  wanachama  wengi wenye uwezo wa kubeba dhamana ya Urais na kuitumikia nchi kwa uzalendo,uadilifu na uaminifu,  hivyo  nafasi ya kiongozi  mmoja kubaki madarakani milele haipo.

"Nafasi zaidi ya miaka mitano ilitolewa kwa Waasisi  Wetu  Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume .Baada ya wao hatatokea yeyote wa kuongeza  muda zaidi ya kuongoza aidha kwa Zanzibar au Tanzania" Alieleza Mwenezi  huyo.


 

Post a Comment

0 Comments