KUWAVALISHA SUTI WAHDZABE,KUHARIBU UTAMADUNI WAO

 Na Ally Mandai

Mbunge wa Katavi, Thomas Maganga, ameieleza Wizara ya Maliasili na Utalii kutoridhishwa kwake na hatua ya kuwavisha suti baadhi ya Wahadzabe waliokuwa wameambatana na Waziri wa Maliasili na Utalii bungeni, akidai hatua hiyo inapunguza uhalisia wa utamaduni wao.
 
Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara hiyo leo Ijumaa Mei 15, 2026, Maganga amesema jamii ya Wahadzabe ni sehemu muhimu ya urithi wa kitamaduni wa Tanzania na ni moja ya vivutio vinavyowavutia watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani.
 
Mbunge huyo amesema haikuwa sahihi kuwabadilisha muonekano wao wa asili kwa kuwavisha mavazi ya kisasa wakati nguvu kubwa inapaswa kuelekezwa katika kuhifadhi tamaduni zao halisi.
 
"Mmeleta Wahadzabe hapa mjini mmewavalisha suti, mnaharibu utamaduni wao. Kuna watu wanatoka Marekani kuja kuwaona katika maisha yao halisi, leo mnawaboresha kwa mtindo ambao si utamaduni wao," amesema Maganga.
 
Aidha, amesisitiza kuwa makabila ya asili yanapaswa kuhifadhiwa katika mazingira na utamaduni wao wa kawaida badala ya kubadilishwa kwa ajili ya shughuli rasmi, akieleza kuwa kufanya hivyo kunaweza kuathiri thamani ya utalii wa kiutamaduni nchini.
 
Katika mjadala huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji, alikuwa ameambatana na baadhi ya wawakilishi wa jamii ya Wahadzabe waliohudhuria bungeni.

 

Post a Comment

0 Comments