KIKWETE APOKEA WATAALAMU KUTOKA SOMALIA KUJA KUJIFUNZA UTAWALA BORA

Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha mafunzo ya utawala bora barani Afrika baada ya kupokea ujumbe wa wataalamu 25 kutoka Somalia kwa ajili ya mafunzo maalumu ya uendeshaji bora wa utumishi wa umma.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya ujumbe huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema hatua hiyo inaonesha imani inayowekwa kwa Tanzania na mataifa mengine kutokana na mafanikio yake katika kuimarisha mifumo ya utawala, amani na utulivu.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo washiriki katika maeneo ya usimamizi wa rasilimali watu, mifumo ya kiutumishi na utoaji huduma bora kwa wananchi kwa haraka na ufanisi zaidi.

Kikwete amesisitiza kuwa mageuzi ya kidijitali yaliyoanzishwa katika Serikali ya Awamu ya Sita yameleta mabadiliko makubwa, yakiwemo kurahisisha huduma za serikali zinazopatikana mtandaoni bila ulazima wa kufika ofisini.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu Xavier Daudi amesema washiriki watajifunza mifumo ya Serikali Mtandao na mbinu za kisasa za utunzaji wa nyaraka.

Naye Mkuu wa TPSC, Ernest Mabonesho, amesema programu hiyo ni matokeo ya makubaliano ya mwaka 2025 kati ya Tanzania na Somalia.

Mshiriki Ayan Andullahi ameipongeza Tanzania kwa mafunzo hayo yanayowaongezea uelewa wa uwazi na uwajibikaji.


 

Post a Comment

0 Comments