MBUNGE MSTAAFU AKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUJIPATIA MALI KWA UDANGANYIFU



NA MWANDISHI WETU

ALIYEWAHI kuwa Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini Yusuph Abdallah Nassir ameachiwa dhamana na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam baada ya kushikiliwa kwa saa kadhaa kwa mahojiano akituhumiwa kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu.

Yusuph ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo hilo mwaka 2010-15 alikamatwa juzi kwa mahojiano maalumu ya tuhuma zinazomkabili ambapo inadaiwa Machi 2024 alijipatia kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kutoka kwa Kampuni ya ATN Petroleum Limited kwa makubaliano ya kuinunulia ardhi maeneo ya Chongoleani Mkoani Tanga kiasi cha hekari 200 kwa lengo la kuwekeza kwenye sekta ya mafuta lakini mtuhumiwa akaenda kinyume na makubaliano.


Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zinaeleza,Mbunge huyo baada ya kuhojiwa aliachiwa kwa dhamana huku upelelezi wa kesi hiyo ukiendelea.Juhudi za kumtafuta Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu kuthibitisha kukamatwa kwa Mbunge huyo ziligonga ukuta kwani simu yake ya mkononi inayoishia na namba mwisho 72 kuita bila kupokelewa kwa siku nzima.

Alipotafutwa mtuhumiwa Yusuph Abdallah Nassir kupitia simu yake mkononi inayoishia namba mwisho 85 alikiri kuwepo kwa kesi hiyo na kampuni ya ATN na kusema shauri hilo limerudishwa kwa Mwanasheria wa Mkoa wa Tanga kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa kisheria.Alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia kwa undani jambo hilo kwa vile lipo katika mamlaka za kisheria na kuomba atafuwe siku nyingine.

Kwa upande wake wakili anayeiwakilisha kampuni ya ATN katika kesi hiyo Fatuma Mwaja alisema,mtuhumiwa Yusuph alipewa fedha hizo kwa ajili ya kununua ardhi lakini akaenda kinyume na makubaliano kwa kujimilikisha eneo hilo kupitia kampuni ya Black Gold Oil and Gas Ltd.


Alisema,ATN Petrolium ilikua imedhamiria kupitia ardhi hiyo kujenga matanki makubwa karibu na mradi wa Bomba la mafuta kama sehemu ya uwekezaji na kutengeneza ajira mpya lakini ndoto hizo zimekwamishwa na mbunge huyo mstaafu kwa kitendo chake cha kujimilikisha ardhi isiyo yake isivyo halali.


Wakili Fatuma alisema,mara baada ya mtuhumiwa kulipwa fedha hizo alirudi mezani kuifuata menejimenti ya ATN na kuomba kua mbia kupitia kampuni yake ya Black Gold Oil and Gas Ltd.Baada ya pande hizo mbili kuafikiana ubia walikubaliana kwamba ardhi inayotakiwa kununuliwa iandikwe jina la ATN Petroleum ambaye ndiye aliyetoa fedha lakini ilipofika Desemba 2025 mlalamikaji akagundua hati ya ardhi iliyonunuliwa imetoka kwa jina la Black Gold Oil and Gas Ltd ambayo ni kampuni ya mtuhumiwa.

Vyanzo vya Habari vinaeleza mtuhumiwa baada ya kuibua sintofahamu hiyo akaenda mbali na kumuingiza Mkurugenzi wa ATN Petroleum Abdulatif Taalib kuwa Mkurugenzi Mwenza katika kampuni ya Black Gold Oil and Gas Limited bila ridhaa ya muhusika.


Alisema,walichukua hatua kumuandikia barua Msajili wa Hati Mkoa wa Tanga wakimuomba abatilishe hati hiyo kwani imetolewa kimakosa wakitaka amilikishwe mteja wao ambao ni kampuni ya ATN.Alisema,mara baada ya kuandika barua hiyo serikali ya Mkoa wa Tanga kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali iliitisha kikao cha pande hizo mbili Februari 18 mwaka huu kujaribu kupatia ufumbuzi mgogoro huo lakini hakikuzaa matunda kutokana na kushindwa kufikiana muafaka.


Wakili Fatuma alisema,walilazimika kuchukua hatua za kufungua kesi Polisi na mtuhumiwa alikamatwa na kuhojiwa kabla ya kuachiwa kwa dhamana.Kuhusu uwepo wa kikao kingine chini ya Wakili Mkuu wa Mkoa wa Tanga,alisema kwa sasa shauri hilo lipo Polisi Kanda Maalumu katika hatua ya upelelezi kabla hatua nyingine za kisheria kuchukuliwa.

Post a Comment

0 Comments