YANGA YAPAA LINDI KUSAKA ALAMA TATU MUHIMU

 Na Ally Mandai.

Klabu ya Yanga SC imeanza safari kuelekea mkoani Lindi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Namungo FC. Kikosi hicho kinaelekea kusini mwa nchi kikiwa na morali ya juu, kikilenga kuendeleza ushindani katika mbio za ubingwa msimu huu.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumapili katika Uwanja wa Majaliwa Stadium uliopo Ruangwa, kuanzia majira ya saa 1:00 usiku. Yanga wanahitaji matokeo chanya katika dimba hilo gumu, huku wenyeji Namungo wakisaka alama muhimu mbele ya mashabiki wao wa nyumbani.

Baada ya kumaliza kibarua hicho cha ugenini, Yanga watasafiri kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya mchezo mwingine wa ligi dhidi ya JKT Tanzania. Mchezo huo utapigwa katika Uwanja wa KMC Complex, ambapo Wananchi watahitaji kuonyesha uthabiti wao katika ratiba ngumu ya mechi mfululizo.

Ratiba hiyo inaipa Yanga changamoto ya kusimamia vyema kikosi chao, hasa katika suala la uchovu na majeraha, ili kuhakikisha wanabaki kwenye kiwango bora katika kila mechi. Benchi la ufundi linatarajiwa kufanya mzunguko wa wachezaji ili kulinda ubora na ushindani ndani ya timu.

Baada ya michezo hiyo miwili ya ligi, macho na masikio ya mashabiki yataelekezwa kwenye dabi kubwa dhidi ya Simba SC itakayochezwa visiwani Zanzibar Machi 1. Dabi hiyo inatarajiwa kuwa ya ushindani mkubwa, huku kila upande ukihitaji ushindi kwa ajili ya heshima na kujiimarisha zaidi katika msimamo wa ligi.







 

Post a Comment

0 Comments