Na Ally Mandai.
Msemaji wa klabu ya Simba SC, Ahmed Ally amezungumza na waandishi wa habari kuhusu kile kinachodaiwa kuwa wamelalamika baada ya mchezo wa dabi kupelekwa Zanzibar.
Kwanza, nikiri wazi kwamba ni kweli tumeandika barua kwenda Bodi ya Ligi. Hata hivyo, si barua ya kulalamika, bali ni barua ya kuomba ufafanuzi wa kikanuni kuhusu baadhi ya masuala yanayohusu mchezo wetu wa tarehe mosi mwezi wa tatu.
Simba ni taasisi kubwa; hatulalamiki. Kwa mantiki hiyo, hatuoni sababu ya kulalamika kwa kuwa hakuna anayetutendea isivyo haki. Tulichoona kinafaa ni kuandika barua rasmi ili kupata ufafanuzi wa kina juu ya mambo machache, kwa mujibu wa kanuni.
Hatukupenda kuyaweka wazi masuala hayo hadharani kwa sababu mechi ya Simba dhidi ya Yanga ni mechi kubwa inayobeba hisia na hatma ya mambo mengi. Kuweka hoja hizo wazi kabla ya majibu ya mamlaka husika kungeweza kuleta taharuki, tafsiri tofauti au hata mtafaruku usio wa lazima, jambo ambalo lingeweza kuathiri taswira ya soka la nchi yetu pamoja na ubora wa Dabi yenyewe.
Kwa hiyo, barua iliwasilishwa Bodi ya Ligi na tayari tumepokea majibu. Tumepatiwa ufafanuzi na mambo mengi yanaendelea vizuri. Kwa sasa hatuna mashaka, isipokuwa masuala ya mwisho ya kuridhia yataongozwa na maelekezo ya viongozi wetu.
Kwa kifupi, tumeandika barua, tumepata majibu, na taratibu zinaendelea kama inavyopaswa.


.jpg)
0 Comments