Mwandishi Wetu, Zanzibar
WATU wanaotaka kununua nyumba, shamba au kiwanja Zanzibar wametakiwa kutokufanya hivyo holela ni vema wakajiridhisha mamlaka husika ili kuondoa sintofahamu inayoweza kujitokeza kwa kutapeliwa kwa kuuziwa eneo ambalo serikali ina mpango nalo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi au hifadhi ya barabara.
Akizungumza Mjini Unguja, Zanzibar Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema Zanzibar wengi wamejenga katika maeneo ambayo hayajapimwa na pia kuna ambayo yametengwa kwa ajili ya uwekezaji hivyo mwenye uhitaji kabla ya kununua anapaswa kwenda wizara husika kujiridhisha.
Alisema pia ni vizuri kwa atakaye ardhi kuwasiliana na Wizara ya Ardhi Zanzibar na atakaye nyumba kuliona Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kwani kutokana na ujenzi holela uliokwisha fanyika, serikali hivi sasa inatumia pesa nyingi kulipa fidia kiasi ambacho kingeweza kutumika kwa ajili ya shughuli zingine za maendeleo.
"Fedha nyingi zinatumika kulipa watu fidia hata Rais Hussein Ali Mwinyi anasema sababu watu tumejenga hovyo, tumeingia hadi service road (hifadhi ya barabara), leo ukimwambia mvunje, anakuambia ooh, mimi sipigi kura, nachoma bendera ya CCM, inahusiana nini na maendeleo?" alihoji Mbeto.
Aliwataka watekelezaji wa miradi kufanya shughuli zao na hata kama sehemu kuna tawi la CCM wavunje maana wananchi wanataka maendeleo.
Alisema CCM ndio inaisimamia serikali na tunataka maendeleo na tumekubaliana na Rais Dkt. Mwinyi, tumeenda siku 46 za Kampeni Uchaguzi Mkuu 2025 na tumewahubiria watu kupata maendeleo, miji mizuri, barabara, elimu na afya njema na mambo yote hayo lazima ujenge miundombinu.
Mwenezi Mbeto alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Mwinyi wa Zanzibar wanaposema uongozi unao acha alama ndio maana yake.
"Namsihi Rais wangu asiogope kusemwa kwani anachokifanya sasa wananchi wataona baadae faida ya kuwa na miji mizuri yenye miundombinu bora" alisema Mwenezi Mbeto.

0 Comments