Na Ally Mandai.
MECHI ya watani wa jadi kati ya Yanga na Simba, maarufu kama Kariakoo Dabi, sasa itapigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar badala ya Dar es Salaam. Mchezo huo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara umepangwa kuchezwa Machi 1, 2026.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amethibitisha taarifa hizo akieleza kuwa Yanga wakiwa wenyeji wameamua kuuhamishia mchezo huo Zanzibar. Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Kabylie katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi.
Hata hivyo, pamoja na ushindi huo, Yanga imeshindwa kusonga mbele hadi robo fainali baada ya kumaliza nafasi ya tatu ikiwa na pointi nane, nyuma ya vinara Al Ahly waliokusanya pointi 10 na AS FAR Rabat waliopata pointi tisa. JS Kabylie wao walimaliza mkiani wakiwa na pointi tatu.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kamwe aliandika: “Mchezo wetu wa Ligi Kuu Machi 1, 2026 dhidi ya Simba SC ‘Kariakoo Derby’ utapigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex saa 2:15 usiku. Karibuni sana.”
Awali, kwa mujibu wa ratiba iliyoboreshwa na Tanzania Premier League Board (TPLB) na kutangazwa Novemba 17, 2025, mchezo huo namba 54 ulipangwa kuchezwa saa 11:00 jioni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Stadium. Hata hivyo, mabingwa hao wa kihistoria wameamua kuuhamishia visiwani Zanzibar.
Ikumbukwe pia kuwa katika ratiba ya awali iliyotolewa Agosti 29, 2025, dabi hiyo ilitarajiwa kuchezwa Desemba 13, 2025, kabla ya kusogezwa hadi Machi 1, 2026 ili kupisha maandalizi ya timu ya Taifa, Taifa Stars, kwa ajili ya michuano ya AFCON 2025 iliyofanyika nchini Morocco kuanzia Desemba 22, 2025 hadi Januari 18, 2026, ambapo Senegal ilitwaa ubingwa kwa kuifunga Morocco bao 1-0 kwenye fainali.

0 Comments