Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF) ameshiriki Mkutano wa 67 wa Mawaziri wa Afya kutoka nchi 9 wanachama za Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) unaofanyika Ezulwini, Ufalme wa Eswatini tarehe 2-3 Februari, 2026.
Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo umejadili mikakati ya kuimarisha mifumo ya afya ya nchi wanachama wa ECSA-HC, hususan kwa kuzingatia mabadiliko yanayoendelea duniani kote yaliyopelekea kupungua au kusitishwa kabisa kwa upatikanaji wa fedha za kufadhili miradi ya afya kutoka kwa wafadhili waliozoeleka.
Katika hotuba akifungua Kikao cha Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi wa ECSA-HC, Dkt. Kikwete alitoa rai kwa nchi hizo kuwa wabunifu katika kubuni na kutafuta vyanzo mbadala vya rasilimali za kifedha ili kuhakikisha kuwa miradi iliyokwishaanza kutekelezwa haitetereki au kufa kutokana na kukoma kwa fedha za wafadhili. “Kama Serikali huwezi kuwaambia wananchi kuwa tunasitisha huduma za afya kwa sababu wafadhili wameacha kutoa fedha. Hapana. Ni wajibu wenu kama watunga Sera kuumiza vichwa na kufanya juu chini kutafuta vyanzo mbadala vya fedha ili wananchi waendelee kupata huduma wanazostahili”, alieleza Dkt. Kikwete.
Alitumia pia fursa hiyo kutoa uzoefu wake jinsi walivyowahi kukabiliana na changamoto za aina hiyo wakati wa uongozi wake ambapo moja ya mbinu walizobuni ni kuimarisha ushirikiano wa kikanda baina ya nchi za Afrika ili kuongeza uhimilivu wa mifumo ya afya, ikiwemo uamuzi wa nchi za ukanda huu kufanya manunuzi ya pamoja ya jumla kwa bei nafuu (bulk-procurement) ya dawa, vifaa tisa na vitendanishi badala ya kila nchi kununua vifaa hivyo kivyake.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
0 Comments