MABAO mawili ya Laurindo Dilson Maria Aurélio 'Depu' na moja la Prince Dube jana yalitosha kuifanya Yanga kuendeleza ubabe katika Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji katika mchezo uliopigwa uwanja wa KMC,Mwenge jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo unaifanya Yanga kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi hiyo huku ukiwaongezea morali kuelekea mechi ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri utakaopigwa Jumamosi hii uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar.
Katika mchezo huo wa jana Dodoma Jiji ni kama walichokoza nyuki baada ya kutangulia kufunga bao dakika ya 41 likiwekwa wavuni na William Edgar ambaye aliwachomoka mabeki wa Yanga na kumchambua kipa Djugui Diarra kabla ya timu hizo kwenda mapumziko.
Kipindi cha kilianza kwa kasi Yanga wakiingia na hasira ya kutaka kusawazisha bao hilo ambapo dakika ya 60 beki wa Dodoma Jiji Andy Bikoko alimuangusha Frank Asink wa Yanga na mwamuzi kuamuru kupigwa mkwaju wa penalti.
Mkwaju huo wa penalti uliwekwa wavuni na Aurélio 'Depu' akimpoteza maboya kipa wa Dodoma Jiji Ally Salim Katoro kabla ya straika huyo mpya wa Yanga kupachika bao la pili kwa kichwa na dakika ya 67 Prince Dube kuhitimisha karamu ya mabao.



0 Comments