DK. SAMIA AMEPANDA MTI WENYE TAFSIRI PANA KWA TAIFA



Na Habibu Mchange

_Muembe alioupanda unasimama kama ishara ya uongozi unaoamini katika mizizi ya umoja, shina la mshikamano, na matawi ya amani na mashirikiano yanayowafikia Watanzania wote

Katika picha yenye nguvu ya historia na ujumbe mzito kwa taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameichagua ardhi badala ya jukwaa, mti badala ya sherehe, na vitendo badala ya maneno, kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa tarehe 27 Januari, 2026. 

Akiwa katika eneo la Bungi Kilimo, Mkoa wa Kusini Unguja, Rais Samia alipanda mti wa Muembe (Mangifera indica) tendo lililobeba maana pana kuliko tukio lenyewe.

Hapa ndipo tafakuri ya taifa inaanza. Kitafakuri hiki hakikuwa kitendo cha mazingira pekee, kilikuwa kitendo cha kuunganisha Taifa.Kama mizizi ya mti inavyojipenyeza ardhini na kuishikilia, ndivyo kitendo hiki kinavyoikumbatia Tanzania nzima Bara na Zanzibar, vizazi vya jana, leo na kesho katika wazo moja kuu, kwamba mustakabali wa nchi hujengwa kwa mambo yanayotuunganisha, si yanayotutenganisha.

Kupanda mti ni lugha ya kimya lakini yenye sauti nzito, ni lugha inayosema umoja bila kupiga kelele. Mti hauulizi unatoka wapi, kabila gani, dini gani au chama gani; kivuli chake ni cha wote, hewa yake ni ya wote, na matunda yake ni ya wote. Hiyo ndiyo tafsiri pana ya kitendo cha Rais Samia kwamba Tanzania bora ni ile inayotoa nafasi, ulinzi na matumaini kwa wote.

Kuzaliwa kwake tarehe 27 Januari, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, kunapata maana ya kitaifa zaidi katika tukio hili. Safari ya maisha ya Rais Samia imekutana na safari ya Taifa.Muembe alioupanda unasimama kama ishara ya uongozi unaoamini katika mizizi ya umoja, shina la mshikamano, na matawi ya amani na mashirikiano yanayowafikia Watanzania wote.Tukiitazama kwa kina, miti ndiyo walimu wakuu wa mshikamano, huwezi kuona mti mmoja ukiunda msitu; 

msitu huundwa na miti mingi inayosimama pamoja, vivyo hivyo, taifa hujengwa na watu wake wanapochagua kushirikiana, kuheshimiana na kuaminiana. Kitendo cha Rais kupanda mti leo ni ishara ya kupanda msitu wa matumaini msitu wa Tanzania inayojengwa kwa upendo, amani na ushirikiano.

Faida za kupanda miti si za mazingira pekee ni faida za kijamii na kitaifa. Miti inalinda vyanzo vya maji, inaboresha hewa, inaleta mvua na utulivu wa mazingira.Lakini pia inaleta utulivu wa jamii, Chini ya mti ndipo watu hukaa pamoja, kushauriana, kupumzika na kupatana. 

Hivyo, kupanda mti ni kupanda pia mazungumzo, uvumilivu na mshikamano wa kijamii.Ndiyo maana kuwa na kiongozi anayependa mazingira ni baraka ya taifa. 

Ni kiongozi anayeona uhusiano wa moja kwa moja kati ya mazingira salama na taifa lenye amani. Anajua kuwa ardhi ikiharibika, watu hugombana; maji yakipotea, migogoro huongezeka; hewa ikichafuliwa, afya hudorora. Kupenda mazingira ni kupenda watu, kupanda mti ni kupanda amaniZaidi ya hapo, huu ni uongozi wa imani kwa vizazi vijavyo. Rais Samia, kwa kupanda mti, anawaambia Watanzania kwamba kesho ni muhimu kama leo. 


Anapanda kitu ambacho hatakifurahia peke yake, bali kitafurahiwa na watoto wa Taifa.Huu ni uongozi unaovuka ubinafsi, unaovuka muda, na unaoamini kuwa Taifa ni safari ndefu ya pamoja.

Katika mantiki hiyo, tukio la Bungi Kilimo linabeba tafsiri moja kubwa:kwamba Tanzania mpya haitajengwa kwa migawanyiko, bali kwa mizizi ya umoja; haitasimama kwa kelele, bali kwa utulivu; na haitadumu kwa maneno, bali kwa vitendo vinavyoishi muda mrefu kuliko wanaovifanya.


Hii ndiyo tafakuri ya leo. Kwamba kama miti inavyounganisha ardhi, maji na hewa ili kuleta uhai, ndivyo uongozi wa busara unavyounganisha watu, maadili na matumaini ili kujenga Taifa imara. Kupanda mti leo ni kupanda Tanzania inayotamani kuishi pamoja, kukua pamoja na kustawi pamoja.

Ni hapo ndipo Taifa huunganishwa.Ni hapo ndipo historia huandikwa kwa mizizi, si kwa wino.


Mwandishi wa Tafakuri hii ni 


HabibuMchange


Mwenyekiti  MECIRA 

 

kituo cha wanahabari watetezi wa Rasilimali na Taarifa. 

anapatikana kwa +255762178678

mchangemchange@gmail.com*

Post a Comment

0 Comments