Wengi wanapofikiria kuhusu mataifa yenye visiwa vingi duniani, mawazo yao huenda moja kwa moja kwa nchi za kitropiki kama Indonesia au Ufilipino. Lakini orodha ya mataifa yenye idadi kubwa ya visiwa inaweza kukushangaza, kwani nchi zenye hali ya hewa ya baridi kama Sweden, Norway na Finland ndizo zinazoshika nafasi za juu kabisa. Kutoka kwenye fukwe za Aktiki hadi kwenye misitu ya Kanada, visiwa vipo kwa maelfu vingine vikiwa na wakazi na miji, vingine vikiwa pori kabisa.
Ni muhimu kuelewa kwamba kila nchi hutumia vigezo vyake katika kuhesabu visiwa. Kulingana na CNTraveller (2025), baadhi ya nchi huhesabu kila kipande cha ardhi kinachozungukwa na maji bila kujali ukubwa wake; nchi nyingine huweka masharti ya kimaeneo au urefu wa pwani ili kuhesabu kisiwa kuwa rasmi. Kwa mfano, Sweden huhesabu kila kipande cha ardhi kilichozungukwa na maji ya bahari kinachozidi mita za mraba 25, wakati Japani, katika sensa yake mpya ya mwaka 2023, ilizingatia tu visiwa vilivyo na fukwe au ardhi ya angalau mita 100.
Pia, maendeleo ya teknolojia ya ramani na satelaiti za kisasa yameleta mabadiliko makubwa katika takwimu hizi. Picha za hali ya juu za satelaiti zimewezesha kugunduliwa kwa visiwa vipya au kurekebisha makosa ya zamani. Takwimu zinazotolewa hapa zinajumuisha visiwa vyote vya asili, viwe na wakazi au la.
Visiwa vya kutengenezwa, miamba ya baharini, na mchanga unaopotea wakati wa mawimbi makubwa ya juu kwa kawaida haviingii katika hesabu rasmi.
Kwa kutumia vyanzo kama WorldAtlas (2020), World Population Review (2025), Global Tourism Forum 2025, na CNTraveller (2025), tunakuletea mataifa 10 yaliyo na visiwa vingi zaidi duniani na sababu za kipekee zinazofanya kila moja livutie.
1. Sweden – Visiwa 267,570
Sweden ndiyo kinara wa dunia kwa idadi ya visiwa, ikiwa na visiwa 267,570. Idadi hii inatokana na njia ya kihesabu inayojumuisha kila kipande cha ardhi chenye ukubwa wa zaidi ya mita za mraba 25 kinachozungukwa na maji.
Hii inaeleza ni kwa nini sehemu kubwa ya visiwa hivi ni vidogo sana na visivyo na wakazi.
Licha ya ukubwa mdogo wa visiwa vingi, Uswidi imeyafanya kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku. Takriban visiwa 1,000 vina wakazi wa kudumu, huku vingine vikiwa maeneo ya kupumzika, kambi, au uvuvi.Mji mkuu Stockholm umejengwa juu ya visiwa 14 vinavyounganishwa kwa zaidi ya madaraja 50.
2. Norway – Visiwa 239,057
Norway, inayojulikana kwa fukwe zake za kuvutia, ina idadi ya visiwa inayofikia 239,057. Jiografia yake ya milima, pwani ndefu, na maeneo ya Aktiki huchangia sana kuwa na wingi wa visiwa.
Norway pia huhesabu visiwa vyake kwa upana zaidi, ikiwa na maeneo mengi ya bahari yenye kingo zilizokatika na miamba inayojitenga na bara.Visiwa maarufu kama Lofoten na Svalbard vina sifa za pekee. Lofoten kina mandhari ya kupendeza ya asili, wakati Svalbard kiko mbali kaskazini karibu na ncha ya dunia. Pia, ukijumlisha visiwa hivi, Norway ina moja ya fukwe ndefu zaidi duniani.
3. Finland – Visiwa 179,854
Finland inajulikana kwa kuwa na maziwa mengi, lakini pia ni mojawapo ya nchi zilizo na visiwa vingi zaidi duniani, visiwa takribani 179,854. Visiwa hivi vipo ndani ya maziwa, mito, na pwani ya Bahari ya Baltic. Kama ilivyo kwa Sweden, visiwa vingi vya Finland ni vidogo na visivyo na wakazi.
Visiwa vya Aland, vinavyofurahia mamlaka ya kujitawala, ni kati ya makundi muhimu ya visiwa nchini humo.Kwa Wafini wengi, kuwa na nyumba ya kupumzika wakati wa likizo kwenye kisiwa au kando ya ziwa mara nyingi ikiwa na sauna ni sehemu ya maisha yao ya kila majira ya kiangazi.
4. Canada – Visiwa 52,455
Kanada, yenye eneo kubwa la kijiografia na bahari tatu zinazozunguka, ina visiwa 52,455. Kutoka visiwa vikubwa kama Baffin Island hadi visiwa vidogo visivyo na wakazi katika maeneo ya Aktiki, Kanada ina tofauti kubwa katika ukubwa, hali ya hewa, na matumizi ya visiwa vyake.
Kisiwa cha Baffin, kwa mfano, ni kisiwa cha tano kwa ukubwa duniani na kina ukubwa mkubwa kuliko nchi nzima ya Uhispania.Visiwa vya Kanada vina faida kubwa kwa mazingira, maisha ya porini, na pia historia ya makabila ya asili.
5. Indonesia – Visiwa 17,500
Indonesia ni taifa linalosifika kwa kuwa na visiwa vingi vinavyokaliwa na watu. Ikiwa na visiwa zaidi ya 17,500 na takriban 6,000 tu vikikaliwa na watu.
Indonesia ni moja ya nchi zenye utofauti mkubwa wa kitamaduni na kibaiolojia duniani. Iko katikati ya ikweta na inajumuisha visiwa maarufu kama Java, Sumatra, Bali, na Kalimantan.
Visiwa vya Indonesia vimeenea kwenye ukanda wa Pasifiki, na taifa hili lina kanda tatu za muda.Maisha ya watu, dini, lugha, na tamaduni tofauti huonyesha jinsi visiwa hivi vinavyochangia katika utambulisho wa taifa hili.
6. Marekani – Visiwa 18,617
Marekani inashikilia nafasi ya sita kwa kuwa na visiwa 18,617. Idadi kubwa ya visiwa hivi vinapatikana katika jimbo la Alaska, ambalo lina mandhari ya porini, baridi kali, na visiwa visivyo na makazi mengi.
Pia kuna visiwa maarufu kama Hawaii, Florida Keys, na visiwa vya Great Lakes.Kisiwa cha Kodiak ni cha pili kwa ukubwa nchini, kikifuatiwa na Big Island ya Hawaii.Licha ya ukubwa wa nchi, visiwa vya Marekani vina utofauti mkubwa kutoka maeneo ya tropiki hadi ya baridi kali.
7. Japani – Visiwa 14,125
Japani ni taifa la visiwa, na sensa ya 2023 ilionyesha kuwa ina visiwa 14,125. Tofauti na mataifa mengine, Japani ilihesabu tu visiwa vyenye pwani ya angalau mita 100 hatua ambayo ilitokana na matumizi ya teknolojia ya ramani ya kisasa.
Visiwa vikuu vinne vya Honshu, Hokkaido, Kyushu, na Shikoku vina asilimia kubwa ya wakazi, lakini visiwa vidogo vimekuwa muhimu kwa utamaduni wa Kijapani, ikiwemo maisha ya uvuvi, mahekalu ya kale, na maumbile ya kipekee.
8. Australia – Visiwa 8,222
Ingawa bara lake ni kubwa, Australia pia ina visiwa 8,222. Visiwa vya Tasmania, Whitsundays, Fraser Island (K'gari), na visiwa katika Torres Strait vinaonyesha utofauti wa visiwa vya nchi hii.K'gari ni kisiwa kikubwa zaidi cha mchanga duniani na ni eneo la urithi wa dunia.
Visiwa vya Australia vina wanyama wa kipekee, uoto wa asili wa kuvutia, na ni sehemu maarufu za utalii wa fukwe, michezo ya majini, na uhifadhi wa mazingira.
9. Ufilipino – Visiwa 7,640
Ufilipino ni mfano kamili wa taifa la visiwa, likiwa na visiwa 7,640, ambavyo kati ya hivyo visiwa takribani 2,000 tu ndivyo vyenye makazi ya watu.
Visiwa vikuu kama Luzon, Visayas, na Mindanao vinachukua sehemu kubwa ya watu, huku visiwa vidogo kama Palawan, Siargao, na Bohol vikivutia watalii kwa fukwe zake za ajabu.
Kwa kuwa vimeenea Bahari ya Pasifiki, visiwa hivi vina mchango mkubwa kwa utamaduni, lugha mbalimbali, na maisha ya kila siku ya watu wake.
10. Uingereza – Visiwa 6,000+
Uingereza haijulikani sana kwa kuwa na visiwa vingi, lakini inakadiriwa kuwa na visiwa zaidi ya 6,000. Mbali na Great Britain na Ireland, kuna visiwa vingi katika katika makundi ya visiwa yakiwemo matatu makubwa; Hebrides, Orkney, na Shetland huko Scotland, na pia visiwa vya pwani ya England na Wales.
Visiwa kama St. Kilda vimetangazwa kuwa Maeneo ya Urithi wa Dunia wa UNESCO kwa sababu ya historia ya kipekee na mazingira yasiyoguswa na maendeleo.
Kwa ujumla idadi ya visiwa kwa kila nchi inategemea jinsi taifa linavyotafsiri kisiwa, pamoja na teknolojia ya kisasa ya ramani. Hii inaeleza kwa nini nchi kama Sweden na Finland zilizo karibu na ikweta zinaongoza kwa idadi ya visiwa.Kila taifa katika orodha hii lina hadithi ya kipekee kuhusu visiwa vyake kuanzia mazingira ya porini hadi maeneo ya kihistoria na kiutamaduni.
@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@



0 Comments