Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Mkoani Manyara, Mheshimiwa Daniel Sillo, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Bashnet kinachoendelea kujengwa katika jimbo hilo.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Sillo alipokelewa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Babati (OCD) Mrakibu waPolisi (SP) Ernesta Mwambinga, ambaye alimpa taarifa ya hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo pamoja na umuhimu wake katika kuimarisha usalama na utulivu wa wananchi wa Bashnet na maeneo ya jirani.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi, Sillo amesema ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa moja ya ahadi alizozitoa kwa wananchi wa Bashnet wakati wa kampeni za uchaguzi, kufuatia maombi ya wananchi waliotaka kusogezewa huduma za kipolisi karibu na maeneo yao.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa kituo hicho kutasaidia kupunguza uhalifu, kurahisisha upatikanaji wa huduma za haki na usalama, pamoja na kuongeza ufanisi wa jeshi la polisi katika wilaya ya Babati.
Mheshimiwa Sillo amewaomba wananchi kutoa ushirikiano wao katika utekelezaji wa mradi huo na kusisitiza kuwa ataendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi, ikiwemo sekta ya usalama, elimu na miundombinu.
Kwa upande wake, SP Ernesta Mwambinga amemshukuru Mbunge Sillo kwa juhudi na msukumo wake katika kuhakikisha kituo hicho kinajengwa, akisema kuwa kitakapokamilika kitaongeza uwepo wa polisi karibu na wananchi na kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao katika Tarafa ya Bashnet na maeneo ya jirani.jfif)
0 Comments