MAFUNZO ELEKEZI KWA WAHESHIMIWA MADIWANI WA LINDI MANISPAA NA KILWA YAFUNGWA RASMI.

 Mafunzo elekezi ya Uongozi kwa madiwani wa Manispaa ya Lindi pamoja na Halmashauri ya Kilwa yaliyolenga kujenga uwezo wa kiuongozi na utendaji wa majukumu yamefungwa rasmi Januari 7,2025 na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Victoria Mwanziva baada ya kudumu kwa muda wa siku tatu.

Akifunga mafunzo hayo Mhe. Mwanziva amewataka madiwani kuyatumia vizuri mafunzo waliyoyapata kwenye jamii zao ili kuleta ubunifu katika utendaji na usimamizi wa majukumu yao ipasavyo, kutetea wananchi na kuongeza chachu ya ubunifu katika utendaji kazi.

Aidha amewahimiza Madiwani kudumisha umoja, upendo na ushirikiano baina yao katika utekelezaji wa shughuli zao ili kuleta ufanisi.

Akitoa neno la utangulizi, Bwn. Juma Mnwele, Mkurugenzi ya Manispaa ya Lindi amewaomba madiwani kutumia mafunzo waliyopata kama alama ya kurejelea wanapohitaji tafsiri, maana au suluhisho katika uongozi wao na kuongeza kuwa serikali inaamini kupitia mafunzo hayo madiwani wameongeza uelewa na ufanisi wa kufanya kazi na wataalamu wa serikali pamoja na kuhudumia wananchi katika maeneo yao.

Ndugu. CPA Florian J. Simon, mratibu wa mafunzo ngazi ya Mkoa amewashukuru madiwani hao kwa kuhudhuria kikamilifu mafunzo hayo yaliyowawezesha kupata elimu na mafunzo ambayo serikali inategemea watakwenda kuyatumia katika kusimamia utendaji kazi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika ngazi ya serikali za mitaa.

Mhe. Hassan Swaleh Yusufu, Diwani wa kata ya Songosongo na halmashauri ya Kilwa kwa niaba ya madiwani wenzake ametoa shukrani za dhati kwa waratibu wa mafunzo hayo kwani yamewapa motisha ya utendaji kazi kwa kuwapatia stadi ya utekelezaji wa majukumu yao na kuhaidi kuyatumia mafunzo hayo kama chachu ya kuleta maendeleo zaidi, kusimamia sheria na kanuni za Utawala Bora.





Post a Comment

0 Comments