WAZIRI WA KILIMO AKABIDHIWA KIFAA CHA KUPOKELEA TAARIFA ZA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA



Dodoma, 16 Desemba 2025

Leo tarehe 16 Desemba 2025, jijini Dodoma, Mheshimiwa Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo, amekabidhiwa kifaa cha kupokelea taarifa za bidhaa zinazokusanywa na kuuzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, ambapo hadi sasa zaidi ya asilimia 85 ya bidhaa zinazotumia mfumo huo ni za kilimo.

Kifaa hicho kimekabidhiwa na Bw. Asangye Bangu, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), kwa lengo la kumwezesha Waziri kupokea taarifa za moja kwa moja (mbashara) kuhusu bidhaa zinazopita katika mfumo huo.

Akizungumza wakati wa kupokea kifaa hicho, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ameonesha kuridhishwa kwake na utendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala na kuitaka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuimarisha zaidi mfumo kwa manufaa ya wakulima na taifa kwa ujumla.

Tukio hilo lilishuhudiwa na Bw. Gerald Mweli, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, ambaye alimjulisha Mheshimiwa Waziri kuwa kanzidata atakayokuwa akiipata kupitia kifaa hicho ni ya moja kwa moja, jambo litakalompa uelewa mpana wa bidhaa zote zinazopita katika Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

Kwa upande wake, Bw. Asangye Bangu alimhakikishia Mheshimiwa Waziri kuwa Bodi itaendelea kufanya kazi kwa bidii kubwa ili kuhakikisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unaendelea kuwa mfumo sahihi na madhubuti wa kuwapatia wakulima tija na thamani halisi ya mazao yao kutokana na jasho lao.

 

Post a Comment

0 Comments