WAZEE WASIOJIWEZA BUKUMBI WAISHUKURU SERIKALI KUIMARISHA HUDUMA ZA USTAWI WAO

 Wazee wanaoishi katika Makazi ya Wazee na wasiojiweza Bukumbi, wilayani Misungwi mkoani Mwanza, wameishukuru Serikali kwa kuimarisha huduma za ustawi wao, wakisema hatua hiyo imeleta faraja, heshima na matumaini mapya katika maisha yao ya uzeeni.

Mwenyekiti wa Wazee  kituoni hapo, Mzee John Nguku amesema wazee wanathamini jitihada Serikali za kuwapatia huduma muhimu kwa wakati. 

“Kwa niaba ya wazee wenzangu, tunaishukuru Serikali kwa kutukumbuka tunaishi kwa amani, tunahudumiwa kwa heshima na tunahisi bado tuna thamani katika jamii, tunaomba uangalizi huu uendelee ili wazee wengi zaidi wanufaike maana uzee siyo mzigo bali ni neema”. amesema Mzee John

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema Serikali inawatambua wazee kama tunu muhimu ya Taifa na itaendelea kuimarisha huduma za ustawi na ulinzi wao.

Mhe. @Maryprisca_mahundi amesema pamoja na jitihada za Serikali, jamii ina wajibu wa msingi wa kuwatunza wazee, huku akiwataka vijana kutowasahau wazazi wao wanapofikia uzee na kuhakikisha wanapata upendo, heshima na msaada unaostahili.

Kwa upande wake, Mfawidhi wa Makazi ya Wazee na wasiojiweza Bukumbi, Vivian Kaiza amesema uangalizi wa Serikali na ushirikiano wa wadau umeendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa wazee waliopo kituoni hapo, Makazi yanaendelea kusimamiwa kwa weledi na kujali maslahi ya wazee, huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha wazee wanapata huduma stahiki na kuishi kwa amani.





Post a Comment

0 Comments