MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesaini hati ya makubaliano na Kampuni ya Africa Global Logistics (AGL) Tanzania Ltd yenye makao makuu yake Ufaransa kwa ajili ya usanifu, ujenzi na uendeshaji wa gati mpya tatu katika Bandari ya Bagamoyo.
Hati hii ya makubaliano imesainiwa jana katika makao makuu ya TPA, Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa na Rais wa AGL ambayo ni kampuni tanzu ya MSC, Philippe Labonne.
Mbossa amesema kusainiwa kwa hati ya makubaliano ni ishara ya utayari wa kuanza kwa mradi wa bandari mpya ya Bagamoyo ambapo kwa kuanzia, AGL itaanza usanifu na ujenzi wa gati tatu mpya za kisasa kati ya 28 zinazotarajiwa kujengwa katika bandari hiyo pamoja na gati mbili mpya za kisasa katika Bandari ya Dar es Salaam.
“Tunategemea kuanza ujenzi wa gati mpya tatu katika Bandari ya Bagamoyo mapema Januari na pia tunawakaribisha wawekezaji wengine wa ndani na wa nje katika mradi huo ambao lengo ni kuleta mapinduzi makubwa katika shughuli za kibandari nchini,” alisema Mbossa.
0 Comments