NATAMANI PAMBANO LA ANGEL BUSHOKE NA VICK KIMODO LIRUDIWE MCHANA KWEUPE.



WAJUKUU zangu Angel Bushoke na Victoria Daniel 'Vick Kimodo' nasikia wamezichapa kavukavu usiku mnene viunga vya uchochoroni.Ni pambano ambalo  halikua rasmi wala  udhamini wowote kutoka kwa wadau wa masuala ya ngumi.

Taarifa nilizonazo hata Shirikisho la Ngumi Tanzania halikua na taarifa za pambano hilo ambalo halikua na promota.Sina taarifa sahihi za nani aliyedundwa kwani mashuhuda wengi wamepatwa na kigugumizi kutoa matokeo ya nani mshindi kwani eneo walilopigania mwanga ulikua hafifu.

Ilikua ngumu kupata takwimu sahihi za ngumi zilizokua zinarushwa ila lugha ya matusi haikua na kizuizi watu kusikia mashambulizi ya kila upande.Sijui nini kimewakuta wajukuu zangu hawa kiasi cha kukosa subira na kuamua 'kuvuana nguo' hadharani.

Hivi mlishindwa kuja kunishtakia babu yenu ili niwasuluhishe katika hilo mnalogombea?Ujinga mtupu.Kama mliona kijijini kwangu Kisiju/Mkuranga ni mbali kuja kunifuata basi mngenipigia simu niongea nanyi kupata suluhu kuliko uamuzi mliochukua kupigana hadharani.

Bahati nzuri nyote namba zangu za simu mnazo.Sijui mlikwama wapi nyie warembo.Lakini pia hapo Dar es Salaam kuna wazee wenzangu wangu wengi ningeweza kuwaelekeza muende mkapate suluhu.Hivi Angel na Model hamjui  kupigana hadharani ni kosa la jinai na mnaweza kushtakiwa na Jamhuri.Mko tayari kupoteza muda wenu kupandishwa kizimbani?

Kabla ya kupigana mlifikiria lolote kuhusu madhara mtakayozipa taasisi mnazozifanyia kazi?
Huyu mmoja ni Makamu Mwenyekiti wa Chamudata mwingine ni dansa wa Twanga Pepeta.
Taasisi zote mbili zinaheshima kubwa katika tasnia ya muziki wa dansi nchini.

Kitendo mlichokifanya hata kama ni masuala binafsi lakini kimezinajisi taasisi zenu.Hapa ndipo ilibidi muongozwe na busara zaidi kuliko hasira.Inawezekana wengi tunawafahamu wawili nyie kama wasanii wa dansi tu lakini kumbe mna kipaji cha ngumi ambacho mmekitambulisha usiku mnene ambapo wengi hawakuwashuhudia.

 Nadhani sasa ni wakati muafaka wa kuwatafutia promota  wa kuendeleza vipaji chenu kipya.Babu yenu nipo tayari kutoa udhamini mnono wa pambano lenu ili lirudiwe mchana kweupe apatikane mshindi halali  tumalize ubishi wa nani mbabe kati yenu.Babu yenu Kionambali nimeumizwa na uhuni mlioufanya wa kupigana hadharani.Natamani mtoke hadharani na kuomba radhi mashabiki wenu bila kujali nani kamkosea mwenzio na ukweli wa tuhuma zenu.

Kionambali M.Kionambali

P.O.BOX 2785

0754-629298

Kisiju/Mkuranga/Pwani

Post a Comment

0 Comments