Leo majira ya saa mbili asubuhi, nilitoka nyumbani Majohe na kwenda katika benki ya CRDB tawi la Gongolamboto.
Baada ya kufika ndani ya benki hiyo, nilipokelewa vizuri sana na mlinzi wa benki hiyo, dada mmoja mrembo wa kampuni ya ulinzi ya Suma JKT. Baada ya kumueleza shida yangu ambayo inahusiana na mambo ya NSSF akanielekeza mahali ninapoweza kuhudumuwa mle ndani.
Wakati akinielekeza, mara akafuatwa na kijana mmoja mdogo sana na mpole mno uso wake ukiwa umesawajika, Kijana yule akaanza kumueleza yule dada mlinzi kuwa anataka kublock akaunti yake ya benki. Dada akamuuliza kwa nini? Ndipo akaanza kuelezea mkasa uliompata akiwa barabarani Gongolamboto nafikiri alikuwa anakuja pale benki.
Kijana akasema alipokuwa njiani alisimamishwa na mtu mmoja na kudai yeye ni polisi na kutoa kitambulisho. Dogo kwa madai yake akakiangalia kitambulisho hicho na kilionyesha kuwa huyo jamaa ni polisi na akamwambia kuwa tunakagua vitambulisho. Anasema wakati amemsimamisha kwa mbele karibu na mahala walipokuwa kulikuwa na polisi wenye uniform hivyo dogo hakuwa na wasiwasi kabisa na anasema jamaa alikuwa anajiamini sanaaaaa! (Hii ni silaha mojawapo muhimu sana ya matapeli).
Basi wakuwa katika mazungumzo mara akapita jamaa mwingine naye akasimamishwa na huyo polisi fake bila shaka huyo ni mshirika wake katika kufanya utapeli.
Polisi fake akamuomba huyu kijana wa chuo kitambulisho akampa. Akamwambia atoe na vitu vingine alivyokuwa navyo, kijana akatoa kadi ya benki ya CRDB akampa na akadai huyo jamaa akamwambia kuwa ampe na namba ya siri ya kadi yake maana anaenda kuvikagua kituoni.
Dogo wa mwaka wa pili wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, akatoa namba ya siri ya akaunti yake akampa yule muhuni! Kisha akamwambia sasa subiri hapahapa naenda kukagua kituoni. Kijana anasema wakati anasemeshwa yote hayo, akili yake ilikuwa kama imehama kabisa alikuwa haelewi kinachoendelea hadi jamaa alipoondoka ndipo akashtuka na kuja moja kwa moja pale benki kutoa taarifa.
Bahati nzuri benki walifanikiwa kublock akaunti yake hivyo wale jamaa kwakuwa ni wajanja na kwakuwa walishapata namba ya siri mya akaunti bila shaka walikuwa wanakimbilia benki nyingine ya karibu ya CRDB labda Banana pale ili waweze kutoa pesa maana walijua fika kwenda kutoa pale tawi la Gongolamboto karibu na mahali walipomtapeli dogo ingekuwa ni hatari kwao.
Nimemsikiliza kwa uchungu sana mwanangu yule kijana mdogo kabisa yaani ukimuangalia unaweza kudhani ni kijana wa kidato cha pili. Mdogo sana yaani na bila shaka tapeli aliingia na uhusika wa hali ya juu sana mpaka kuweza kumrubuni dogo hadi kuweza kumpa nyaraka zake zote hizo muhimu ikiwemo kadi ya benki na namba ya siri ya akaunti yake.
Katika mjadala ule pale baada ya dogo kueleza hivyo, watu wakasema kuwa hao jamaa inasemekana kuwa pia huwa wanatumia sana mambo ya mazingara!
Nilichojifunza hapa ni kuwa pamoja na kuwa matapeli wapo kila siku, lakini pia wanabuni mbinu mpya kila siku.
Angalia jamaa kaenda kumtapeli dogo akiwa jirani kabisa na polisi walio katika doria mitaani na pia siyo polisi tu waliokuwa eneo hilo bali pia kulikuwa na wanajeshi wa jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania ambao pia wanaimarisha ulinzi na usalama maeneo mbalimbali ya jiji kutokana na matukio ya hivi karibuni, lakini yule muhuni kaweza kumsimamisha dogo na kujieleza kuwa yeye ni polisi na dogo akawa na imani naye kutokana na jinsi jamaa alivyojiamini na kutoa kitambulisho fake na dogo pia kuona kuwa polisi wapo karibu na eneo la tukio hilo ambapo huyo muhuni alikuwa anatekeleza vitendo vyake vya "usanii"!
Matapeli wapo kazini kwa mbinu za hali ya juu kabisa kama mbinu hiyo aliyotumia huyo jamaa kumsimamisha dogo karibu kabisa na vyombo vya dola. Huyu aliyemtapeli dogo kusema kweli katumia mbinu kali kabisa ya kusimamisha karibu na vyombo vya ulinzi na usalama ili kumtoa dogo hofu. Kajua kabisa kuwa wakiwa jirani na vilipo vyombo vya dola itakuwa rahisi kwake kutekeleza mipango yake na hii ni kutokana na kuwa kila mtu yupo katika pilikapilika zake hivyo mtu huwezi kujua nini kinaendelea.
Matapeli wanaweza kutumia fursa ya namna ya hali ilivyo kwa sasa na kutekeleza uhalifu kwa kivuli cha kujifanya polisi kama huyo tapeli aliyemtapeli dogo mwanafunzi wa chuo.
Kila mara inabidi kuchukua tahadhari ndugu zangu maana watu wana mbinu nyungi sana na ni za hali ya juu mno. Imagine mtu ana kitambulisho cha polisi sasa so watu wote wanaweza gundua kuwa hivyo ni vitambulisho fake na mtu mwenyewe pia ni polisi fake.
Maka Patrick Mwasomola,
NSSF Ubungo Plaza,
Kinondoni,
Dar es salaam.
Desemba 4, 2025
0 Comments