KUMEKUCHA HALE FESTIVAL DESEMBA 26,HALE TANGA



NIMESOMA mtandaoni ujio wa onesho kubwa la dansi kwa ajili ya kuaga mwaka 2025.Ni lile litakalozikutanisha bendi kongwe za muziki wa dansi nchini Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' na watani zao Mlimani Park Orchestra 'Sikinde Ngoma ya Ukae' litakalofanyika Desemba 26 mwaka huu Hale Lounge,Mkoani Tanga.
Ni tamasha maalum kwa ajili ya kumuenzi aliyekua mwanamuziki nguli wa bendi ya Msondo Ngoma marehemu Ally Muhoja Kishiwa TX Moshi William anayekaribia kutimiza miaka 20 ya maadhimisho ya kifo ambapo bendi hizo zitaoneshana kazi jukwaani.

Hakika Babu yenu Mzee Kionambali M.Kionambali nimevutiwa na ujio wa onesho hilo lenye sura na ladha tofauti na vile ambavyo tumezoea.Maonesho yenye kuzikutanisha bendi hizo yamezoeleka  kufanyika jijini Dar es Salaam tu.Bendi hizo hazijakutana nje ya Jiji la Dar es Salaam muda mrefu hivyo ni zilikuwa  zinawanyima haki  mashabiki wake waliojaa nchi nzima.

Wajukuu zangu wa Hale wamefanikiwa kufanya mapinduzi ya kimuziki kwa kuleta burudani hiyo yenye sura ya kitaifa Mkoani Tanga.Waandaji wameamua kubadilisha mandhari kutoka Dar es Salaam na sasa shughuli ya mtoto hatumwi dukani siku hiyo imeshushwa Mkoa wa waja leo waondoka leo.

Hale ni pembezoni kidogo mwa Jiji la Tanga.Ni mji wenye mkusanyiko wa makabila mengi uliochangamka mno kibiashara sambamba na kujengeka kuendana na kasi ya maendeleo ya nchi.Wajukuu zangu Hassan Msumari,Ally Kileo na wengine wanaoijua Hale ni mashuhuda wa sifa njema za mji huo wenye hali ya hewa ya kiubaridi tulivu.

Hakika waandaji hawakukosea kuileta burudani hiyo Hale kutokana na mji huo kukidhi hadhi ya kupokea ugeni mkubwa wa wadau wa muziki wa dansi kutoka kila pembe ya nchi.

Hakika Hale ipo  tayari kuwapokea mashabiki wa Msondo na Sikinde kwa mara ya kwanza katika jukwaa moja.Naifahamu vyema Hale kwakuwa Babu yenu Kionambali  mke wangu wanne(yaani bibi yenu) anatoka hapo na nilifunga naye ndoa mwaka 1988.

Unaweza kuona umbali wa kutoka kijijini kwangu Kisiju, Mkuranga, Pwani hadi kuja kuopoa chombo Hale.Licha mandhari nzuri ya mji huo pia umejaaliwa kumiliki hazina ya mabinti warembo haswa.

Kwa wajukuu zangu vijana kwao ni fursa adhimu ya  kutakasa macho kabla ya kusogelea lengo la kuachana na ukapera. Naam hakika Hale imejaaliwa neema nyingi zinazoweza kukufanya ukaloea  baada ya onesho hilo na kujikuta ukifanya Utalii wa ndani.

Babu yenu nimeanza kudunduliza fedha mpaka Desemba 25 niwe Hale tayari kwa kushuhudia burudani ya Msondo na Sikinde nje ya viwanja vyao vya nyumbani.Kwa bahati nzuri onesho hili limekuja msimu wa mavuno huku Kisiju kwahiyo fedha ya malazi na chakula kwangu haiwezi kuwa shida.

Siwezi kuiacha burudani ya Msondo na Sikinde nje ya Jiji la Dar es Salaam inipite kirahisi.Licha ya uzee wangu wa miaka(87)nilionao lakini nasema nitajikongoja kwenda Hale siyo kwa ajili ya kwenda kuwasalimia wakwe zangu bali ile burudani ya Msondo na Sikinde ndiyo itakayonipeleka huko.

Nitashangaa kuona wewe mdau wa muziki wa dansi unaachaje kufunga mwaka na shoo yenye ladha mpya.Twendeni Hale wajukuu zangu tukapate burudani ya muziki wa dansi sambamba na kujionea mandhari nzuri ya mji huo.Nimesikia taarifa zisizo rasmi baadhi ya wajumbe wa Kamati za Ufundi wa bendi hizo tayari wako Hale wakipita maeneo mbalimbali kuweka mambo sawa maana inaelezwa kila mmoja amepania kumtoa nishai mwenzie jukwaani.

Kionambali M.Kionambali

S.L.P 2785

Kisiju/Mkuranga Pwani

0754-629298


 

Post a Comment

0 Comments