Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania yataka wananchi kufunga kwa siku tatu


 Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania(JMAT), imetoa tamko la kuomba kufanyika maombi ya kitaifa yatakayotanguliwa na mfungo wa siku tatu kuanzia ALHAMIS wiki hii ili kuliombea Taifa kutokana kadhia iliyotokea Octoba 29,2025,wakati wa uchaguzi mkuu nchini iliyosababisha hasara za watu kupoteza maisha, uharibifu wa mali za serikali na watu binafsi pamoja na uharibifu wa miundombinu.


Aidha, jumuiya hiyo imepinga vikali baadhi ya viongozi wa dini waliotoa maneno makali yanayoashiria uwepo wa vita na ugomvi kati ya waislamu na wakristo nchini kitu ambacho sio kweli.

Akitoa tamko la Jumuiya hiyo Desemba 3,2025 mbele ya waandishi wa habari Jijini Dodoma, Mwenyekiti wa JMAT, Sheikh Dkt.Alhad Mussa Salum,amesema kadhia hiyo imesababisha kuzaa chuki na athari ya kisaikolojia katika akili na mioyo ya watu na kuleta hisia za udini jambo ambalo linatakiwa kushughulikiwa mapema.

Amesema maombi hayo yawe ya kina kwa watu wa imani na madhehebu mbalimbali na yaratibiwe na kufanyika kitaifa kwa namna moja na siku moja nchi nzima.

Pia imeomba yafanyike maridhiano ya kisiasa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukaa na viongozi wa vyama vya siasa pamoja na uwakilishi wa viongozi wa dini wanaoaminika katika kuwa na fikra njema,huru na misimamo thabiti ili kuunda mwanzo mpya wa kuimarisha mifumo ya kusaidia kuongoza nchi kwa kuaminiwa na wote.

JMAT inawasihi na kuwaomba watanzania hasa vijana kuona uzito wa yale yaliyotokea na namna yalivyogharimu Taifa,hivyo wanawasihi kutoshiriki tena katika yale yanayosemekana kupangwa kufanyika Disemba 9,2025,ambayo ni siku ya heshima nchi ilipopata Uhuru.

Pamoja na maombi hayo JMAT imempongeza kwa dhati na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Dkt.Samia Suluhu Hassan,na serikali yake kwa kulifungua kanisa la ufufuo na uzima na kusema hatua hiyo ni muhimu katika kuleta ustawi wa serikali na waumini wa dini mbalimbali.

Katibu Mkuu wa JMAT Askofu Dkt.Israel Maasa ameshauri kudhibitiwa kwa matumizi ya mitandao ambayo yameonekana ni njia kubwa iliyotumika kusambaza uharibifu na mambo makubwa yaliyojitokeza kwenye vurugu hizo.

Post a Comment

0 Comments